Ulimwengu wa Spoti, Juni 21
Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....
Iran yainyuka Iraq
Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran ameipongeza timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kuinyuka Iraq bao 1 bila jibu katika mchuano wa timu za Asia wa kusaka tiketi ya Kombe la Dunia mwaka ujao 2022 nchini Qatar, na Kombe la Asia litakaloandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Asia (AFC) nchini China mwaka 2023. Katika mchuano huo wa Jumanne usiku, Team Melli ya Iran iliibamiza Iraq na kuvuna alama tatu zilizoibeba na kuifanya ituame kileleni kwa Kundi C. Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran amesema timu hiyo ya soka ya Iran licha ya kupitia mazito, kama vile kuzuia kuwa mwenyeji wa baadhi ya mechi zake, lakini imefanikiwa kumaliza ngwe ya pili ya mechi hizo za Asia za kusaka tiketi ya Kombe la Dunia na mashindano ya AFC nchini China mwaka 2023.

Katika mchezo huo wa usiku wa kuamkia Jumatano, vijana wa Iran waliitandaza vizuri ngozi, huko goli la mshambuliaji mahiri, Sardar Azmoun likitosha kuwasokeza mbele kwa alama tatu za ziada za haraka haraka. Sasa Iran inasogea mbele kwa madaha ikiwa na alama 18. Wiki iliyopita, Iran iliinyoa bila maji Cambodia kwa kuichabanga mabao 10-0, katika mchuano mwingine wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao 2022 nchini Qatar.
Taekwondo; Iran mshindi wa 3 Asia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa tatu katika Mashindano ya Ubingwa wa Taekwondo Barani Asia yaliyofanyika huko Lebanon. Katika mashindano hayo yaliofanyika baina ya Juni 14 na 16 katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, wanataenwondo wa Iran walizoa jumla ya medali 13, zikiwemo mbili za dhahabu. Korea Kusini imeibuka kidedea katika mashindano hayo ya kieneo kwa kutia kibindoni medali sita za dhahabu, tano za fedha na shaba nane, huku nafasi ya pili ikitwaliwa na Uzbekistan kwa kuzoa medali tatu za dhahabu, moja ya fedha na sita za shaba.

Dhabau za Iran zilitwaliwa na Sajad Mardani aliyeng'ara katika safu ya wanataekwondo wenye kilo zaidi ya +87 safu ya wanaume, na Negar Esmaeili kategoria ya akina dada wenye kilo zisizozidi -46. Makumi ya wanataekwondo wa kutoka nchi za bara Asia wameshiriki kwenye mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama The 2021 Asian Taekwondo Championships yaliyororoma katika Uwanja wa Nouhad Naufal katika eneo la Zouk Mikael, nje kidogo ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Mieleka; Iran yang'ara Uturuki
Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika huko Uturuki. Katika mashindano hayo yaliyong'oa nanga Juni 18 na kufunga pazia lake Jumapili hii ya Juni 20 mjii Istanbul, wanamieleka wa Iran walitwaa medali kochokocho katika kategoria tofauti. Kwenye mashindano hayo yaliyopewa jina la Vehbi Emre & Hamit Kaplan, Iran ya Kiislamu ilizoa medali tatu za dhahabu, mbili za fedha na mbili za shaba. Vijana wa Iran waliyolitea fahari taifa hili kwa kuzoa medali za dhahabu ni Sajjad Abbaspour, Mohammadreza Mokhtari na Ramin Taheri katika safu za wanamieleka wenye kilo 55-, 72-, na 87-kg kwa usanjari huo. Nao Pouya Dadmarz na Hossein Assadi walishinda medali za fedha kila mmoja katika kategoria ya kilo 55- na 67, with Meisam Delkhani kitwaa fedha katika kundi la wenye kilo 63, na Muirani mwenziwe Amin Kavianinejad katika kitengo cha kilo 72.
Ligi ya Mabingwa Afrika
Wikendi hii kumepigwa mechi mbili kali za hatua ya nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika na kushuhudia Kaizer Chiefs na Al Ahly zikiibuka na ushindi ugenini. Kaizer ikiwa ugenini nchini Morocco kwenye Dimba la Mohamed V, ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Samir Nurkovic dakika ya 34 kwa shuti kali dhidi ya Waydad Casablanca anayoichezea Mtanzania Saimon Msuva. Kaizer ilifika nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa bao 4-3 dhidi ya Simba mwezi Mei mwaka huu kwenye mechi za robo fainali ikishinda 4-0 nyumbani na kupoteza kwa kufungwa 3-0 ugenini kwenye Dimba la Mkapa. Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia dhidi ya Al Ahly ya Misri na kushuhudia Ahly ikishinda 1-0, ugenini kwenye uwanja wa Stade Olympique de Rades.
Ahly kwenye hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu ilikuwa kundi moja na Simba iliyomaliza kinara wa kundi lao na timu hizi mbili zilipokutana Simba ilishinda 1-0, Februari 23, nyumbani kabla ya mechi ya marudiano iliyopigwa Aprili 9, nchini Misri na Ahly kushinda 1-0. Mechi za marudiano baina ya timu hizo zilizotinga nusu fainali msimu huu zimepangwa kupigwa Juni 26 ambapo Kaizer watakuwa nyumbani kwao Afrika Kusini dhidi ya Wydad wakati Ahly watakuwa wakiwakaribisha Esparence huko Misri. Ahly ndiye bingwa mtetezi wa kombe hilo pia ndio Mabingwa mara nyingi katika historia ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika wakiwa wamebeba kombe mara tisa.
Mchujo TFF
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewatema baadhi ya wagombea wa urais wa shirikishi hilo, kwa kukosa kutimza vigezo ilivyovianisha. Kupitia makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Benjamin Kalume, Hawa Mniga, Evans Mgeusa na Rais anayetetea kiti chake Wallace Karia ndio wagombea waliokidhi vigezo vya kugombea nafasi ya Urais wa TFF, huku wagombea wakipigwa nje katika mchujo huo wa awali. Wagombea wanaosemekana wameshindwa kukidhi vigezo kadhaa ikiwemo cha kukosa wadhamini ni pamoja Ally Mayay na mwandishi wa habari za spoti, Oscar Oscar. Ally Mayay, amekiri kuwa amestahili kukatwa katika kinyang’anyiro hicho kutokana na kutofikisha idadi ya wadhamini watano waliotakiwa. Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mayay amefafanua kuwa aliwasilisha vitu vyote vinavyotakiwa ikiwamo vyeti lakini upande wa wadhamini hawakukamilika. Ameeleza kuwa amejitahidi kuomba udhamini katika klabu zote 18 za Ligi Kuu Tanzania Bara ila mmoja ndiye iliyomuunga mkono. Uchaguzi huo mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania unatazamiwa kufanyika Agosti 7 jijini Tanga.
Michuano ya Uropa
Mechi za Mashindano ya 16 ya Soka ya Ulaya (EURO 2020) zinaendelea kushuhudia, huku baadhi ya miamba ya soka barani humo ikionyeshwa chamtema kuni. Ujerumani walitoka nyuma na kuwapokeza Ureno ambao ni mabingwa watetezi wa Euro kichapo cha mabao 4-2 katika mechi ya Kundi F iliyowakutanisha uwanjani Allianz Arena mnamo Jumamosi. Matokeo hayo yaliweka wazi Kundi F kwa kikosi chochote kuibuka kileleni. Ujerumani na Ureno sasa wanajivunia alama tatu kila mmoja huku Ufaransa waliolazimishiwa na Hungary sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya Jumamosi, wakidhibiti kilele kwa pointi nne. Mshambuliaji na nahodha Cristiano Ronaldo aliwafungulia Ureno ukurasa wa magoli katika dakika ya 15 kabla ya beki Ruben Dias wa Manchester City kusawazishia Ujerumani alipojifunga katika dakika ya 35. Bao la pili la Ujerumani pia lilitokana na Ureno kujifunga kupitia kwa Raphael Guerreiro kunako dakika ya 39. Magoli hayo mawili yalichochea motisha ya Ujerumani waliofunga mabao mawili mengine ya haraka kupitia kwa Kai Havertz na Gosens katika dakika za 51 na 60 mtawalia. Bao la Ronaldo anayechezea Juventus lilikuwa lake la tatu kufikia sasa kwenye kampeni za Euro mwaka huu na la 12 katika historia yake ya kushiriki kipute hicho cha bara Ulaya. Ronaldo sasa amepachika wavuni magoli 107 akivalia jezi za timu ya taifa ya Ureno ambao wamemwajibisha mara 177. Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid sasa amesalia na magoli mawili pekee kumfikia Ali Daei wa Iran ambaye mabao yake 109 kimataifa ndiyo rekodi ya dunia. Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia sasa watakamilisha kampeni zao za Kundi F dhidi ya Hungary mnamo Juni 23 huku Ureno wakivaana na Ufaransa.

Kwengineko, fowadi na nahodha Robert Lewandowski alifunga bao lake la kwanza kwenye fainali zinazoendelea za Euro na kusaidia timu ya taifa ya Poland kuwalazimishia Uhispania sare ya 1-1 ambayo iliweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora. Poland walijibwaga ugani wakijua kwamba wangekosa kusonga mbele kutoka Kundi E iwapo wangezidiwa maarifa na Uhispania waliowekwa kifua mbele na Alvaro Morata katika dakika ya 25. Baada ya kushindwa kutambisha Poland katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi E ulioshuhudia Slovakia wakisajili ushindi wa 2-1 mnamo Juni 14, Lewandowski anayechezea Bayern Munich alijituma vilivyo na akasawazisha dhidi ya Uhispania katika dakika ya 54.
Huku hayo yakijiri, nyota Antoine Griezmann aliwavunia Ufaransa alama moja na kuwanyima Hungary ushindi muhimu ambao ungekuwa wa kihistoria kwenye soka ya Euro wakati wa mchuano wa Kundi F uliowakutanisha mnamo Jumamosi mbele ya mashabiki 60,000 jijini Budapest. Nayo Uingereza na Scotland waliambulia sare tasa kwenye mchuano wa Euro wa Kundi D uliowakutanisha uwanjani Wembley mnamo Ijumaa usiku mbele ya mashabiki 22,500. JAMHURI ya Czech ilijiweka pua na mdomo kufuzu kwa hatua ya 16-bora kwenye fainali zinazoendelea za Euro baada ya kuwalazimishia Croatia sare ya 1-1 mnamo Juni 18, 2021 uwanjani Hampden Park.
……………………..TAMATI……………..