Ulimwengu wa Spoti, Jul 5
Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....
Iran kutuma mnyanyua uzani wa kwanza mwanamke Olimpiki
Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kunyanyua Uzani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itamtuma Parisa Jahanfekrian kuwa mwanamke wa kwanza kuliwakilisha taifa hili katika katika mchezo huo wa kunyanyua vitu vizito katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo huko Japan. Ali Moradi amesema, licha ya kufanyiwa upasuaji siku chache zilizopita, lakini mwanadada huyo wa Kiirani akiwa chini ya uangalizi wa makocha na timu ya madaktari, ataiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu huko Tokyo na kuwa mwanamke wa kwanza wa Kiirani kushiriki mchezo huo katika ngazi ya kimataifa.
Binti huyo wa Kiirani mwenye kilo 87 amesema anaona fakhari kubwa kuteuliwa kuliwakilisha taifa lake kama mwanamke wa kwanza wa Kiirani kushiriki mchezo huo wa kunyanyua uzani mzito katika Olimpiki. Amesema jeraha la bega alilokuwa nalo limeshapona baada ya kufanyiwa upasuaji, na kwamba anatumai atafanya vyema huko Tokyo.
Iran yaibuka ya 2 mieleka ya vipofu Uturuki
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa pili katika Duru ya Nne ya Mashindano ya Kimataifa ya Vijana ya Mieleka ya Greco-Roman kwa wanamieleka wenye matatizo ya kuona. Katika mashindano hayo yaliyofanyika Jumamosi mjini Istanbul nchini Uturuki, wanamieleka wa Iran walitwaa medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba. Dhahabu ya Iran ya Kiislamu ilitwaliwa na Amir Mohammad Gholinia katika kategoria ya wanamieleka wenye kilo 87, huku Mojtaba Malekabadi akitunukiwa medali ya fedha katika safu ya wanamieleka wenye kilo 63. Medali mbili za shaba za Iran zilitiwa kibindoni na Ali Vatan Parast na Mostafa Yahyaei katika kitengo cha kilo 55 na kile cha kilo 60 kwa usanjari huo. Russia imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kiingereza kama World Deaf Junior Greco Roman Wrestling Championships, huku mwenyeji Uturuki ikifunga orodha ya tatu bora kwenye mashindano hayo.
Soka: Iran yajua mahasimu
Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu imewafahamu washindani wake katika itakaovaana nao katika duru ya tatu na ya mwisho ya michuano ya kusaka tiketi ya kutinga fainali za Kombe la Dunia zinazopigwa mwaka ujao 2022 nchini Qatar. Katika droo iliyochezwa Alkhamisi jijini Kuala Lumpur nchini Malaysia, Iran imepangwa katika Kundi A pamoja na Korea Kusini, Iraq na Umoja wa Falme za Kiarabu Syria na Lebanon. Kundi B inazijumuisha Japan, Australia, Saudi Arabia, Oman, China, na Vietnam.
Michuano hiyo ya kusaka tiketi za kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar mwakani inatazamiwa kupigwa Septemba 2 na 7, Oktoba 7 na 12, na Novemba 11 na 16 mwaka huu 2021, na vile vile Januari 27 na February Mosi mwakani, kabla ya kufika kilele chake Machi 24 na 29, mwaka ujao 2022.
Mama Samia ashuhudia Deby la Kariakoo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan siku ya Jumamosi alijimwaya mwaya katika Uwanja wa Mkapa kushuhudia debila Kariakoo, mchezo wa Simba dhidi ya Yanga, ambapo Young Africans walipata ushindi hafifu wa bao 1-0 lililofungwa na Zawadi Mauya. Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Samia kuhudhuria mechi ya Ligi Kuu Bara tangu awe Rais wa Awamu ya sita. Mara baada ya kuwasili Rais Samia alikwenda moja kwa moja juu kuketi huku maelfu ya mashabiki wa timu zote wakimshangilia kwa kelele sambamba na kumpigia makofi. Rais Samia alipokelewa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallece Karia akiwa amekaa naye pamoja katika eneo la wageni maalum. Kuwasili kwa Rais Samia kunafuta ratiba ya awali ambayo ilikuwa inamfanya Waziri wa Maji Juma Aweso kuwa mgeni rasmi kama ilivyotangazwa mapema na timu mwenyeji wa mchezo wa Jumamosi Simba. Wekundu wa Msimbazi walijikuta wakipoteza mchezo huo, baada ya mabeki wake kuruhusu goli la kizembe katika kipindi cha kwanza. Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC Haji Sunday Manara, amewashukia baadhi ya Mashabiki na Wanachama wanaosaka visingizio, baada ya timu yao kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Young Africans jana Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wamekua wakimlalamikia Mwamuzi Emmenuel Mwandembwa kwa kuwepa video fupi kwenye mitandao ya kijamii, inayoonesha beki wa Young Africans Dickson Job akizuia mpira kwa mkono uliopigwa na Morisson, huku wakudai ilikua penati halali, ambayo haikukubaliwa na Mwamuzi huyo kutoa Arusha.
Debi la Mashemeji Kenya
Huko nchini Kenya, debi la mashemeji lilishuhudiwa siku ya Jumapili katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, ambapo Gor Mahia iliisasambua AFC Leopard mabao 4-1. GOR wamemaliza ukame wa miaka tisa bila taji la Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka Kenya maarufu kama Betway Cup baada ya kuzima mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards kwa njia ya penalti 4-1 ugani Nyayo, Jumapili. Vijana wa kocha Vaz Pinto, ambao kufuatia ushindi huo wamefuzu kushiriki Kombe la Mashirikisho la Afrika msimu 2021-2022, walionekana kidogo kuwa chini kimchezo katika muda wa kawaida wa dakika 90, lakini walionyesha ustadi katika upigaji wa penalti. Gor, ambayo mara ya mwisho ilikuwa imeshinda kombe ni mwaka 2012 kupitia penalti 3-0 dhidi ya Sofapaka, ilipokea tiketi ya soka ya CAF pamoja na zawadi ya Sh2 milioni. Leopards iliridhika na tuzo ya Sh1 milioni. Bidco United iliyobwaga Equity Bank 1-0 katika mechi ya kutafuta nambari tatu, ilitia mfukoni Sh750,000 nayo Equity ikaridhika na Sh500,000.
Michuano ya Uropa 2020
Mashindano ya 16 ya Soka ya Ulaya (EURO 2020) yanaelekea ukingoni. Katika mchuano wa kusisimua wa robofainali ya michuano hiyo, Italia iliifunga Ubelgiji mabao 2-1 na kutinga nusu fainali. Ubelgiji na Italia zilikabiliana kwenye robo fainali katika uwanja wa Allianz huko Munich, Ujerumani. Italia ilifunga dakika ya 31 kupitia mchezaji Nicolo Barella aliyetuma mpira kwenye wavu kwa shuti lake na kuiweka timu yake mbele kwa 1-0. Katika dakika ya 44, Italia iliongeza bao la pili kupitia Lorenzo Insigne na kufanya matokeo kuwa 2-0. Katika dakika ya 45, Ubelgiji ilipata penalti baada ya Giovanni Di Lorenzo kumcheza vibaya dhidi ya Jeremy Doku kwenye eneo la hatari. Romelu Lukaku alifunga dakika ya 45 + 2 na kugeuza matokeo kuwa 2-1. Italia ilishinda mechi hiyo 2-1 na ikawa mpinzani wa Uhispania katika nusu fainali. Mechi ya nusu fainali kati ya timu hizo mbili itachezwa London, mji mkuu wa Uingereza, siku ya Jumanne, Julai 6.
Huku hayo yakijiri, Uingereza pia imetinga nusu fainali baada ya kuipepeta Ukraine 4-0 katika Mashindano ya 16 ya Soka ya Uropa (EURO 2020) na kutinga nusu fainali. Ukraine na Uingereza zilikabiliana katika robo fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Olimpiki huko Roma, mji mkuu wa Italia. Katika pambano hilo, mabao ya Uingereza yalifungwa na Harry Kane dakika ya 4 na 50, Harry Maguire dakika ya 46 na Jordan Henderson dakika ya 63. Uingereza itamenyana na Denmark kwenye nusu fainali itakayochezwa siku ya Jumatano, Julai 7, katika Uwanja wa Wembley ulioko mji mkuu wa London.
Dondoo za Olimpiki
Wanariadha wa Namibia, Christine Mboma na Beatrice Masilingi wameondolewa katika mashindani ya mbio za Mita 400 za Olimpiki za Wanawake baada ya vipimo kuonesha wana viwango vya juu vya homoni aina ya ‘Testosterone’. Wawili hao walitazamiwa kuwa miongoni mwa wagombea medali, lakini vipimo vilivyofanywa katika kambi yao ya mazoezi huko Italia vimepelekea waondolewe. Caster Semenya (Afrika Kusini), Francine Niyonsaba (Burundi) na Margaret Wambui (Kenya) wameshindwa kushiriki mbio za Mita 800 baada ya kukataa kushusha viwango vya homoni hizo kwa kutumia dawa.
Wakati huohuo, mwanariadha wa Marekani Sha'Caari Richardson ameenguliwa kushiriki mbio za Mita 100 kwenye michuano ya Olimpiki 2020 ambayo itaanza Julai 23 mwaka huu Tokyo nchini Japan. Sababu zilizopelekea mwanadada huyo kuenguliwa ni baada ya kufanyiwa vipimo na kubainika kuwa anatumia bangi. Kwenye mahojiano na NBC, Richardson (21) amesema aliamua kutumia bangi ili kuondoa mawazo baada ya Kifo cha mama yake mzazi.
……………………..TAMATI……………