Jul 18, 2021 02:37 UTC
  • Jumapili 18, Julai, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 7 Dhul Hija 1442 Hijria Qamaria inayosadifiana na 27 Tir Hijria Shamsiya sawa na tarehe 18 Julai 2021

Tarehe 7 Dhulhija miaka 1328 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir", yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).

 

Tarehe 18 Julai, ni "Siku ya Kimataifa ya Mandela". Mwaka wa 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku hii kuwa siku mahsusi kwa Nelson Mandela, mwasisi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Umoja wa Mataifa uliitangaza siku ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, yaani tarehe 18 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ya Mandela ili kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati ya kupigania uhuru nchini Afrika Kusini na juhudi zake kubwa za kutangaza amani, kutilia maanani utatuzi wa migogoro baina ya kaumu na nchi mbalimbali, kutetea haki za binadamu, na kuwepo usawa na maelewano baina ya wanadamu wa mbari na kaumu zote. Mandela alifariki dunia tarehe 5 Disemba mwaka 2013.

Shujaa Mandela

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita,  Zuheir Muhsin, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya al Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa mashirika ya ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) na lile la Misri huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Maajenti wa tawala hizo mbili walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo. Zuheir Muhsin alikuwa mpinzani mkubwa wa mapatano ya kisaliti ya Camp David na aliwahi kutishia mara kadhaa kwamba harakati yake ya al Sa'iqa itamuua mtawala wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadaat aliyetia saini makubaliano hayo na Wazayuni.

Zuheir Muhsin

Miaka 240 iliyopita katika siku kama ya leo, William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia. Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo. Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.

William Herschel

Siku kama ya leo miaka 1150 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9. Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896.