Jul 30, 2021 22:08 UTC
  • Jumamosi, 31 Julai, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1442 Hijria sawa na tarehe 31 Julai 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1314 iliyopita alizaliwa Imam Mussa al Kadhim ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Alilewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kuchota elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kingi cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii ya leo. ***

 

Tarehe 31 Julai miaka 215 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza. Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa. ***

Ardhi ya Cape nchini Afrika Kusini

 

Miaka 135 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary. Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt. ***

Franz Liszt

 

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight." ***

Antoine de Saint-Exupery

 

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo. Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi. Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad. ***

Elijah Muhammad

 

Na tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama hii ya leo miaka 34 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka. Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Iran na mahujaji wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Kiwahabi ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia Mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 wa Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja.

Taswira ya mauaji dhidi ya Mahujaji