Jul 31, 2021 21:56 UTC
  • Jumapili, Agosti Mosi, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 21 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1442 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Agosti 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita , sawa na tarehe 21 Dhulhija mwaka 1329 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Akhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani, mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu wa Iran. Baada ya kuhitimu elimu yake ya mwanzo mwanazuoni huyo alisoma katika vyuo mashuhuri vya kidini vya Iran na Iraq na kupata umashuhuri mkubwa katika elimu za fiqhi na usuli. Akhund Khorasani alifundisha na kulea wanazuoni wakubwa na mashuhuri kama Sayyid Abul Hassan Isfahani, Sayyid Abul Qasim Kashani, Sayyid Muhammad Taqi Khansari, Sayyid Hassan Mudarris, Sheikh Abdul Kariim Hairi, Mirza Hussein Naini na wengine wengi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mashuhuri ni 'Kifayatul Usul' ambacho hadi sasa ni kati ya vitabu vyenye hadhi kubwa katika somo la usulul fiqhi na kinafundishwa kwenye vyuo mbalimbali vya kidini. ***

Ayatullah Akhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani

 

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979. ***

Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya

 

Miaka 16 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.***

Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia

 

Na tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama. Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.***

Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama