Aug 03, 2021 02:01 UTC
  • Jumanne tarehe 3 Agosti 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 23 Mfunguo Tatu Dhulhija 1442 hijria sawa na tarehe 3 Agosti mwaka 2021.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel.

Izzuddin Qalq

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ya Niger iliyoko magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru kutoka kwa Ufaransa. Kuanzia karne ya 18 Niger ilianza kuwa chini ya Ufaransa, na ulipofika mwaka 1922 Paris ilianzisha kambi za kijeshi nchini humo. Niger inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abbas Qummi, aalim na mpokeaji hadithi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum huko kusini mwa Tehran. Sheikh Abbas Qummi alianza kusoma elimu ya dini akiwa huko huko Qum na baadaye alielekea katika chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf nchini Iraq ili kukamilisha masomo yake. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Sheikh Abbas Qummi alipata elimu kutoka kwa maulamaa watajika wa hauza hiyo ya kielimu. Sheikh Abbas Qummi alirejea Iran baada ya muda ambapo alitumia muda wake wote kuandika vitabu na kufuatilia masuala ya kidini. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni Mafatiihul Jinan na Manazilul Akherah.

Ayatullah Sheikh Abbas Qummi

Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, meli ya kwanza ilipita katika Mfereji wa Panama na kwa utaratibu huo, mfereji huo ukawa umefunguliwa rasmi.  Wahandisi wa Kifaransa ndio walioanza kujenga mfereji huo wa Panama na baadaye Wamarekani walikamilisha kazi hiyo. Kujengwa mfereji huo wenye kilomita 68, kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.

Siku kama ya leo miaka 529 iliyopita, ilianza safari kubwa zaidi ya uvumbuzi ya baharia wa Kiitalia Christopher Columbus.  Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya ya kuelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania wa wakati huo. Kwa sababu hiyo Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Wakati huo Columbus na wenzake walidhani kuwa wamewasili India lakini walikuwa wamevumbua bara America bila ya wao kujua.

Christopher Columbus