Jumapili, Agosti 8, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 28 Dhul Hijja 1442 Hijria Qamaria sawa na Agosti mwaka 2021 Miladia
Siku kama ya leo miaka 2354 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.***
Tarehe 28 Dhulhija siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah. Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.

Miaka 22 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.***
Na Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, alifariki dunia Hadi Sabzavari au Hajj Mulla Hadi Sabzavari, mmoja wa maulama na wanafalsafa wakubwa wa karne ya 13 Hijiria. Mulla Hadi Sabzavari alizaliwa mwaka 1212 Hijiria ambapo umri wake ulijaa baraka, huku mwishoni mwa maisha yake akijawa na izza ya nafsi, zuhdi na ucha-Mungu. Athari za Mulla Hadi Sabzavari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Waislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'an, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba. Aidha Mulla Hadi Sabzavari mbali na kufikia daraja za juu za kielimu, alikuwa pia malenga. Katika uwanja huo, alikuwa akisoma mashairi ambayo yalifungamana na nukta za kifalsafa na elimu ya irfani. Allamah Iqbal Lahore, malenga na mwanafalsafa mkubwa wa Pakistan, alimzungumzia Mulla Hadi Sabzavari kuwa, mwanafikra mkubwa wa Iran ambaye falsafa yake alijifunza kupitia dini ya Kiislamu. Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikami' na 'al-Jabru wal-Ikhtiyaar.'