Aug 10, 2021 02:26 UTC
  • Jumanne tarehe 10 Agosti 2021

Leo ni tarehe Mosi Mfunguo Nne Muharram mwaka 1443 Hijria sawa na Agosti 10 mwaka 2021.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu. Kabla ya kalenda ya Miladia kutumika kote duniani, nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa zikitumia kalenda ya Hijria Qamaria.      

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita yaani tarehe Mosi Muharram mwaka wa 7 tangu Mtume (saw) abaathiwe na kupewa utume kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu, Makuraishi walifunga mkataba wa kuweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake. Viongozi wa makafiri wa Makka ambao walikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kasi ya kustawi Uislamu na vilevile kutokana na kufeli njama zao za kuzuia kuenea dini hiyo, waliamua kuweka mzingiro wa kiuchumi ili kufanikisha malengo yao. Kwa msingi huo waliamua kuweka mkataba dhidi ya Waislamu. Mkataba huo uliwakataza watu wote kufanya muamala wa aina yoyote na wafuasi wa dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake walizingirwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika bonde lililojulikana kwa jina la Shiibi Abi Twalib wakisumbuliwa na matatizo mengi na mashinikizo ya kiuchumi na katika kipindi hicho Mtume (saw) alipoteza wasaidizi wake wawili muhimu yaani ami yake, Abu Twalib na mkewe kipenzi, Bibi Khadija. Waislamu hao walisimama imara kulinda imani yao na hawakutetereka hata kidogo licha ya matatizo makubwa waliyokabiliana nayo. Mzingiro huo wa kiuchumi dhidi ya Waislamu ulikomeshwa mwezi Rajab mwaka wa kumi baada ya kubaathiwa Mtume.

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon.

معاهده سور

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China.

Vita vya China na Japan

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya Zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ya Korea yalidhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.

 

Tags