Jumatano tarehe 13 Oktoba 2021
Leo ni tarehe 6 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 13 Oktoba 2021.
Siku kama ya leo miaka 2559 iliyopita mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Kurosh, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Kurosh aliamuru kubadilishwa mkondo wa Mto Tigris uliokuwa ukipita katikati ya mji wa Babel. Kwa utaratibu huo askari wa Kurosh walitumia njia ya zamani ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji wa Babel. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa, ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.
Katika siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Joseph Arthur Gobineau. Gobineau alizaliwa mwaka 1816 mjini Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Aidha Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na kuhusiana na suala hilo akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu. Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan.
Siku kama hii ya leo miaka 57 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord). Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.
