Jumamosi, 16 Oktoba, 2021
Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 16 Oktoba 2021.
Siku kama ya leo tarehe 9 Rabiul Awwal miaka 1183 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SWT) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wacha-Mungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu. ***
Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka, malikia wa Ufaransa Marie Antoinette kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 aliyekuwa mume wa Antoinette, miezi 10 kabla ya hapo alikuwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa ni na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa.***
Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita alizaliwa huko Dublin Ireland, Oscar Wilde mwandishi mashuhuri Kiireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na Chuo Kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya visa vya Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince).
Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo la kuasisiwa shirika la FAO lilikuwa ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula. ***
Na katika siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 43 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya vikosi vya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la vikosi vya usalama vya Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.***