Jumanne tarehe 23 Novemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 17 Rabiuthani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Novemba 2021.
Tarehe 23 Novemba miaka 148 iliyopita, Hanoi mji mkuu wa Vietnam, ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Ufaransa. Tukio hilo lilijiri wakati wa vita vya Ufaransa vya kutaka kuzikoloni nchi za India na China. Tangu katikati mwa karne ya 19, Ufaransa ilikuwa ikifanya njama na jitihada za kuongeza makoloni yake suala lililoifanya nchi hiyo pia kuamua kuuvamia mji huo. Hadi mwaka 1885 askari wa Ufaransa waliikalia na kuidhibiti ghuba ya Tonkin na Vietnam. Hatimaye vikosi vya Ufaransa vililazimika kuondoka huko Vietnam mwaka 1954 baada ya kushindwa vibaya katika vita hivyo.
Miaka 109 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ayatullah Sheikh Muhammad Ali Nakhjavani mmoja wa maulama watajika na wapokezi wakubwa wa hadithi aliaga dunia huko Karbala nchini Iraq. Alikuwa mtu wa Nakhjavan katika Azerbaijan ya leo na alijifunza Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baadaye alijifunza elimu za zama hizo kwa wanazuoni wakubwa. Mwanazuoni huyo alifanikiwa kufikiwa daraja ya Ijitihad na kuwa Marjaa Taqlidi wa Waislamu hususan wa eneo la Caucasia. Ayatullah Nakhjavani ameandika vitabu kadhaa vikiwemo vya Sherhe ya Rasaail na Makasib. Alizikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf.

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave).
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, yaani tarehe 23 Novemba mwaka 1996, ndege ya abiria ya Ethiopia iliyokuwa imetekwa nyara ilianguka katika fukwe za Bahari ya Hindi huko nchini Comoro baada ya kuishiwa na mafuta. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 767 ilikuwa na abiria 175. Abiria 125 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi.