Dec 16, 2021 23:36 UTC
  • Ijumaa tarehe 17 Disemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 12 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 17 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 490 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na pia katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Aidha kitabu cha 'as-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.

Siku kama ya leo miaka 243 iliyopita, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza. Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia. Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829 Miladia.

Humphrey Davy

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.

Wilbur na Orville Wrights

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita mwili wa Mhandisi Muhammad Jawad Tundguyan, waziri wa mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejeshwa nchini Iran kutoka Iraq baada ya kupita miaka 11. Waziri Tundguyan na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo walitekwa nyara na wanajeshi wavamizi wa Iraq wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea visima vya mafuta vya kusini mwa Iran. Waziri huyo na wenzake walitekwa nyara mwezi mmoja baada ya Iraq kuvamia ardhi ya Iran. Utawala wa Saddam wakati huo uliendelea kukanusha kutekwa nyara Mhandisi Tundguyan kwa muda fulani, lakini hatimaye ulikiri kumteka nyara waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran. Uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na watu waliokuwa karibu na Waziri Muhammad Jawad Tundguyan ulithibitisha kwamba waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na kuteswa vikali na askari jeshi wa utawala wa Baath wa Iraq.

Muhammad Jawad Tundguyan

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1992 utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina. Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao. 

Na tarehe 17 Disemba miaka 11 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia aliyejulikana kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.

Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kwa sasa anapewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Tariq Mohamed Bouazizi