Jumatano, Disemba 22, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 17 Mfunguo Nane, Jamadil Awwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 22 Disemba mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 2167 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania.

Siku kama ya leo miaka 1152 iliyopita, yaani mwaka 291 Hijiria, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad bin Yahya Thaalab, mtaalamu maarufu wa lugha na nahau. Abul-Abbas alibobea katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu na baada ya miaka kadhaa ya kufanya utafiti wa kina, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wataalamu mkubwa na magwiji katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zilizobakia kutoka kwa mtaalamu huyo, ni kitabu maarufu cha 'I'raabul-Qur'an', "Qawaaidul Shiir" na "Kitabul Fasiih".

Siku kama ya leo miaka 993 iliyopita, alizaliwa Muhammad Ghazali msomi wa fiq'hi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu wa Iran. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo akiwa na umri wa miaka 28. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo, Khawaja Nidham al-Mulk kumualika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Imam Muhammad Ghazali aliandika kitabu chake maarufu cha "Ihyau Ulumud-Din," mwaka mmoja kabla ya kurejea Iran. Vitabu vingine mashuhuri vya msoni huyo ni "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."
Miaka 382 iliyopita katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699.
Katika siku kama ya leo miaka 328 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Kanali ya Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Kanali ya Suel, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri ya kutangaza kutaifisha kanali hiyo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo, na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.*
Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa. Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.