Dec 23, 2021 02:49 UTC
  • Alkhamisi tarehe 23 Disemba 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 23 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1115 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Kitabu mashuhuri zaidi ya msomi huyo ni al Iqdul Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi.

Katika siku kama ya leo miaka 993 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 96 iliyopita mji wa Jeddah ulitekwa na Ibn Saud na kwa msingi huo utawala wa ukoo wa Hashemi ukahitimishwa katika mji huo. Baada ya kusambaratishwa uasi wa Mawahhabi katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 ,kundi hilo liliendelea kuwachochea watu dhidi ya serikali ya utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 20, Abdul Aziz ibn Abdulrahman ibn Saud, kinara wa moja kati ya makabila ya Hijaz aliamua kuteka moja ya maeneo ambayo yalikuwa yanatawaliwa na Ukhalifa wa Uthmaniyah ambayo alidai eti yalikuwa yameghusubiwa. Kwa msingi hyuo mwaka 1906, baada ya kutea eneo la Riyadh, alijitangaza kuwa mtawala wa eneo hilo. Baada ya hapo watawala wa Uthmaniya walimpa eneo la Al Ahsa la masahriki wa Hijaz na akapata tamaa ya kuendelea kuteka maeneo mengine. Mwaka 1924, Shariff Hussein, Amiri wa Makka ambaye alikuwa kutoka katika ukoo wa Hashemi, alijitangaza Khalifa na hapo Abdul Aziz ibn Saud kwa kisingizo kuwa Amiri alikuwa amejipachika cheo asichostahiki, alianza vita dhidi yake na katika uasi wake huo alifanikiwa kupata uungaji mkono wa makabila na mashekhe wa Kiwahhabi. Hatimaye Disemba 23 mwaka 1925 Miladia, Ukoo wa Hashemi ulisalimu amri na 8 Januari 1926, Abdul Aziz ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa eneo lote la Hijaz. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi na kuundwa rasmi Ufalme wa Saudi Arabia  mnamo September 18 mwaka 1932.

Sura ya sasa ya mji wa Jeddah

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya kimataifa huko Tokyo mji mkuu wa nchi hiyo. Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani kwa ajili ya kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 15 kati yao walihukumiwa kwenda jela.

Waziri mkuu wa zamani wa Japan

Tarehe 23 Disemba miaka 68 iliyopita mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Russia ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrenty Pavlovicha Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali. Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.

Lavrenty Pavlovicha Beria

Siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba miaka 8 iliyopita mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia, Mikhail Kalashnikov ambaye alivumbua bunduki mashuhuri ya Kalashnikov ambayo inajulikana kama AK-47. Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini. Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya. Uundwaji silaha hiyo  ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47.

Mikhail Kalashnikov

Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013 alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini. 

Tags