Jumanne tarehe 28 Disemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 23 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 28 mwaka 2021
Miaka 136 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja miongoni mwa maulama watajika na mahiri mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India. Vilevile ameandika vitabu na makala nyingi.

Katika siku kama ya leo miaka 247 iliyopita yaani mwaka 1774, Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza alifanikiwa kugundua gesi ya oksijeni. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Gesi ya oksijeni ina mchango na nafasi muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na viumbe vingine hai na huingia katika mwili wa mwanadamu wakati wa kupumua na kuchanganyika na chakula. Matokeo ya kazi hiyo ni kuzalishwa nishati ambayo hutumika katika kubakia hai mwanadamu. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.
Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1895 kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa ya filamu, filamu ya kwanza ya kisa ilioneshwa kwenye mkusanyiko wa watu wengi. Filamu hiyo ilitayarishwa na kuandaliwa na ndugu wawili waliojulikana kwa majina ya Auguste na Louis Lumiere. Miaka iliyofuata ilitengenezwa mitambo bora zaidi ya kurekodi na kuonesha filamu na hatua kwa hatua filamu zenye ubora wa juu na za aina mbalimbali zikaanza kuonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani.
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Disemba 1925 alizaliwa Apolo Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda. Obote aliiongoza Uganda kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza mwaka 1962. Aliiongoza Uganda akiwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1962 hadi 1966. Milton Obote alikuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1966 hadi 1971 na kuondolewa madarakani na Idi Amin Dada. Hata hivyo mwaka 1980 alirejea madarakani baada ya Idi Amin kuondolewa uongozi na kuiongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 wakati alipoondolewa madarakani na kulazimika kukimbilia Tanzania na baadaye Zambia. Obote alifariki dunia mwaka 2005 huko Johannesburg Afrika Kusini kwa matatizo ya figo.
Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Dei 1353 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Ayatullah Hussein Ghaffari mmoja wa wanazuoni na mwanamapambano wa Kiislamu. Ayatullah Ghaffari aliuawa shahidi akiwa katika jela ya utawala wa wakati huo wa Kifalme hapa Iran. Ayatullah Ghaffari aliendesha harakati za kupambana na utawala wa kidikteta wa Mfalme Shah kwa kuandika vitabu na majarida mbalimbali. Baadaye alitiwa mbaroni na kutiwa jela na kufa shahidi katika siku kama ya leo, baada ya kuvumilia mateso mengi gerezani humo.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 7 Dey mwaka 1358 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa amri ya kuanzishwa harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Imam Khomeini alitoa amri kwa wananchi wote wa Iran kushirikiana bega kwa bega kwa shabaha ya kumtokomeza adui ujinga. Hivi sasa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika nchini Iran kimeongezeka sana, na kufikia hatua kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuiondoa Iran kwenye orodha ya nchi zisizojua kusoma na kuandika na kuiweka kwenye kundi la nchi zenye watu wengi wenye kujua kusoma na kuandika.
