Dec 30, 2021 23:18 UTC
  • Ijumaa tarehe 31 Disemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 31 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1827 kibiriti kilivumbuliwa na John Walker mtaalamu wa madawa wa Uingereza. Hata hivyo awali, mbali na kibiriti cha Walker kuwaka kwa taabu na mashaka kilikuwa pia na hatari kwa watumiaji wake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wataalamu wengine wakafanya jitihada za kukikamilisha kibiriti hicho. Hatimaye mwaka 1855 mtaalamu mmoja wa Kiswedeni alifanikiwa kutengeneza kibiriti kama hiki kinachotumiwa leo hii baada ya kufanya majaribio na utafiti wa muda mrefu.

Miaka 146 iliyopita katika siku kama ya leo Arthur Christensen mtaalamu wa masuala ya Mashariki alizaliwa huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark. Christensen alionyesha hamu kubwa ya kujifunza masuala ya Mashariki hususan historia ya Iran na mwishoni mwa masomo yake, alifanya utafiti kuhusu historia ya fasihi ya Irani. Arthur Christensen aliweza kujifunza vyema lugha ya Kifarsi. Mojawapo ya vitabu vyake muhimu ni kile alichokipa jina la "Iran katika Zama za Wasasani." Christensen aliaga dunia mwaka 1945.

Arthur Christensen

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja kati ya wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h. Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, huko katikati mwa Iran, katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko Najaf, Iraq. Akiwa huko, alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama Allamah Mirza Shirazi na kupata daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa, irfan na fiq’hi. Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasiilatun-Najjat” na “Tanbiihul-Ummah wa Tanziihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini,

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita iliundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kote duniani, kujenga uhusiano baina yao, kunyanyua juu kiwango cha shule za kidini, kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza baina ya wafusi wa Ahlul Bait na madhehebu nyingine za Kiislamu na kadhalika.

Tarehe 10 Dei miaka 27 iliyopita yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1994 Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kazi kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo. Matangazo ya Idhaa hii yalianza sambamba na sherehe ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika.

Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service.

Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin. Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi. Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa. Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.

Boris Yeltsin

 

AIR