Jumanne, tarehe 4 Januari, 2022
Leo ni Jumanne tarehe Mosi Jamadithani 1443 Hijria inayosadifiana na Januari 4 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 449 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'. Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka ya kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo. Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyodumu kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya.

Tarehe 4 Januari miaka 379 iliyopita alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia kanuni tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi. Isaac Newton aliaga dunia mwaka 1727.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika.
Tarehe 14 Dei miaka 43 iliyopita wakati wa kilele cha harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah, Jenerali Robert E. Huyser aliyekuwa mshauri mkuu wa kijeshi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Marekani aliwasiri kwa siri mjini Tehran. Jenerali Huyser alikuwa na jukumu maalumu la kuisaidia serikali ya Marekani katika kuchukua maamuzi ya baadaye na kupata habari za ndani za Iran katika kipindi cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika kipindi chote cha zaidi ya siku 30 za kuwepo kwake mjini Tehran Jenerali Huyser alikutana mara moja tu na Shah na katika kikao hicho iliainishwa saa na siku ya kuondoka Shah nchini Iran.
Tarehe 4 Januari miaka 11 iliyopita alifariki dunia Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga wa Tunisia, siku 18 baada ya kujichoma kwa moto katika mji wa Buzid akilalamikia ukandamizaji na dhulma ya serikali ya nchi hiyo.
Kujichoma moto kijana huyo muuza mboga kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa nchi hiyo na kuwa sababu ya kupinduliwa dikteta Zainul Abidin bin Ali. Kitendo hicho cha Bouazizi pia kilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.