Jan 09, 2022 23:22 UTC
  • Jumatatu tarehe 10 Januari 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 7 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 10 mwaka 2022.

Miaka 918 iliyopita katika siku kama ya leo, arifu mkubwa wa Kiislamu Ainul Qudhaat Hamedani mwenye lakabu ya Abul Fadhl, aliuawa shahidi kwa kunyongwa huko Hamedam. Alikuwa fakihi, mwanafasihi, msomi na malenga mahiri. Ainul Qudhaat alizaliwa mwaka 492 Hijria. Msomi huyo katu hakuwa akiogopa kubainisha itikadi yake. Ni kutokana na misimamo yake hiyo thabiti ambapo mwaka 525 Hijria alitiwa mbaroni na kufungwa huko Baghdad. Baada ya muda alihamishiwa Hamedan na kunyongwa kando na shule yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Tamhiidat na Haqaiqul Qur’an.

Ainul Qudhaat Hamedani

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita inayosadifiana na 10 Januari 1824, Joseph Aspdin mwanakemia wa Uingereza alifanikiwa kutengeneza saruji na kwa utaratibu huo kupatikana mabadiliko makubwa katika shughuli za ujenzi. Hatua hiyo ilitambuliwa kama tukio kubwa katika shughuli za kimaendeleo na ujenzi mpya wa nyumba. Joseph Aspdin ambaye alikuwa akifanya utafiti kwa miaka kadhaa ili kutengeneza mada ambayo ingesaidia kuimarisha msingi wa nyumba, hatimaye alifanikiwa kutengeneza saruji baada ya majaribio chungu nzima.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo.

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita yaani tarehe 19 Jamadut-Thani mwaka 1360 Hijria, aliaga dunia Ayatullah Abu Abdullah Zanjani mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alimu huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 51 na kuzikwa mahala alipozaliwa yaani Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alijifunza elimu za fasihi, falsafa na itikadi akiwa kijana mdogo. Baadaye Ayatullah Zanjani alielekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Historia ya Qur'ani, Historia ya Maisha ya Mtume Muhammad SAW na Adhama ya Hussein bin Ali ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Zanjani vyenye thamani kubwa.

Ayatullah Abu Abdullah Zanjani

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elekroniki. Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine.