Jumanne tarehe 11 Januari 2022
Leo ni Jumanne tarehe 8 Jamadithani 1443 Hijria sawa na tarehe 11 Januari 2022.
Siku kama ya leo miaka 697 iliyopita mji wa Mexico ambao hivi sasa ni mji mkuu wa nchi ya Mexico, uliasisiwa na mmoja wa wafalme wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa miongoni mwa makabila ya Wahindi Wekundu wa Amerika ya Latini ambao waliwasili huko Mexico katika karne ya 12 na kutawala eneo hilo mwanzoni mwa karne hiyo.
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamili, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Ayatullah Sharafuddin alizaliwa mwaka 1290 Hijria huko Kadhimain moja kati ya miji ya Iraq. Alielekea Jabal Amil nchini Lebanon baada ya kuhitimu masomo yake na kuanza kujishughulisha na harakati za Kiislamu. Msomi huyo mkubwa ametoa huduma za thamani kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa akisisitiza suala la umoja baina ya Waislamu. Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin ameandika vitabu na risala nyingi ili kufikiwa lengo hilo.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita aliaga dunia Ustadh Abulqassim Sahab, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya jiografia na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria Shamsiya katika mji wa Tafresh nchini Iran. Abulqassim Sahab alijifunza fiqih na usul kwa maulamaa wa mji huo na mbali na kupata elimu hiyo alizungumza pia lugha za Kiingereza na Kijerumani.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita sawa na tarehe 11 Januari mwaka 1992, Rais Shazli bin Jadid wa Algeria alijiuzulu baada ya Harakati ya Uokovu wa Kiislamu ya Algeria (FIS) kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa na matukio ya baadaye nchini humo. Rais Shazli alichaguliwa kuwa rais wa Algeria mwaka 1979 baada ya kifo cha Houari Boumediene, rais wa zamani wa nchi hiyo. Mwaka 1988 Shazli bin Jadid aliahidi kutekeleza marekebisho na kufanya mabadiliko ya katiba ya Algeria, ambapo kwa mujibu wake suala hilo lingetoa mwanya wa kutambuliwa rasmi vyama vya kisiasa.
Miaka 10 iliyopita katika siku kama hii ya leo msomi wa nyuklia wa Iran, Mustafa Ahmadi Roshan aliuawa shahidi na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Ahmadi Roshan alikuwa msomi wa nne wa nyuklia wa Iran kuuawa na magaidi wa Israel na washirika wake. Mbali na kujishughulisha na masuala ya nyuklia msomi huyo alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya elimu na sayansi. Ahmadi Roshani aliuawa yeye na dereva wake mjini Tehran akiwa njiani kueleka kazini kwake. Siku kadhaa baadaye genge la magaidi waliomuua msomi huyo wa nyuklia wa Iran na wenzake lilitiwa nguvuni na wanachama wake wakakiri kuwa wana uhusiano na utawala haramu wa Israel na kwamba walipewa mafunzo na maajenti wa utawala huo haramu kwa ajili ya kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran.