Jan 17, 2022 22:17 UTC
  • Jumanne tarehe 18 Januari 2022

Leo ni Jumanne tarehe 15 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 18 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1407 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina. Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali bin Abi Twalib na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu. Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Tarehe 15 Jumadithani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 672 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameandikavitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

Siku kama ya leo miaka 333 iliyopita alizaliwa mwandishi na mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa, Charles de Montesquieu. Alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola. Kitabu maarufu zaidi cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva. Katika kitabu hicho alichunguza aina mbalimbali za serikali zilizojitokeza katika kipindi chote cha historia, ada na sheria za kimaumbile, sheria za kibinadamu na uhusiano baina yao. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni "Persian Letters" (Barua za Kiiran). Alifariki dunia mwaka 1755. 

Charles de Montesquieu

Tarehe 18 Januari miaka 107 iliyopita 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Lengo kuu la mtakaba huo lilikuwa ni suala la kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa.

Georges Clémenceau