Jan 20, 2022 02:10 UTC
  • Alkhamisi tarehe 20 Januari 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 20 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 919 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu. Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake. Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu. 

Miaka 856 iliyopita katika siku kama ya leo kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo. Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587.

Salahuddin al Ayyubi

Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussain Nuri. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani tukufu na mashairi na mwandishi aliyebobea wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu. Mirza Hussain Nuri alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul-Beiti wa Mtume (saw). Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi na miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha "Mustadrakul Wasaail", "Maalimus Sabr", "Jannatul Maawa" na "Nafasur Rahman". Mirza Hussein Nuri amezikwa katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. 

Hajj Mirza Hussain Nuri

Tarehe 20 Januari miaka 102 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".

Federico Fellini

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi.

Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran.

Imam Ruhullah Khomeini

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Ahmad Khansari