Apr 15, 2022 02:22 UTC
  • Ijumaa tarehe 15 Aprili 2022

Leo ni ijumaa tarehe 13 mwezi mtukufu wa Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Aprili 2022.

Siku kama ya leo miaka 1348 iliyopita inayosadifiana na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi, liwali katili na dhalimu katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliishi katika kipindi cha Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, na alikuwa mashuhuri kwa kuwatesa na kuwauwa wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj Thaqafi ni pamoja na kushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba katika mwaka 74 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 570 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya Kanisa Kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.

Leonardo da Vinci

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kugharibi katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza ikielekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa akisema kuwa haiyumkini kughariki na kuzama. Wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 ndio waliookoka katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo duniani.

Titanic

Miaka 36 iliyopita katika siku kama leo, Marekani iliishambulia miji ya Tripoli na Benghazi nchini Libya. Kisingizio kilichotumiwa na Washington kufanya mashambulizi hayo ya anga ni kuwa Libya ilihusika katika mlipuko uliotokea kwenye mkahawa mmoja mjini Berlin, Ujerumani ambapo askari watatu wa Marekani waliuawa. Raia kadhaa ambao hawakuwa na hatia yoyote waliuawa katika mashambulizi hayo ya Marekani katika miji ya Tripoli na Benghazi. Mashambulizi hayo yaliamsha hasira za Waislamu na kulaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala bandia wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.

Khalil al Wazir

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha, vipingamizi vya biashara na kuondoa vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake ilianza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.