Apr 20, 2022 22:17 UTC
  • Alkhamisi tarehe 21 Aprili mwaka 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 21 mwaka 2022.

Miaka 1403 iliyopita, katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Imam Ali bin Abi Talib (as) ambaye ni mkwe, binamu na mtu wa karibu sana kwa Mtume Muhammad SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya kichwani akiwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri katika Msikiti wa Kufa huko Iraq. Imam Ali alipigwa upanga na mtu aliyejulikana kwa jina la Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali (as) alikufa shahidi siku tatu baadaye. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili mkubwa katika Uislamu baada ya Mtume Muhammad (saw) na anaelezwa katika historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa wa kupigiwa mfano, mwenye imani thabiti, akhlaki njema, elimu na uadilifu uio na kifani. Alipata elimu na kulelewa katika nyumba ya Mtume Muhammad (saw), na alikuwa mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali (as) alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali (as) alikuwa mpole na mwenye upendo. Imam Ali daima alitetea haki na uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima, Imam Ali bin Abi Twalib anasema: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake."

Siku kama ya leo miaka 1193 iliyopita, Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza alichukua madaraka baada ya vita vya muda mrefu. Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiongozwa na wafalme wa kiukoo huku ikiwa imegawika katika sehemu kadhaa za kijiografia na kila mtawala akitawala eneo lake maalumu. Egbert aliyekuwa mfalme wa Wessex, eneo lililokuwa Kusini mwa Uingereza ya sasa, baada ya kupambana na watawala wa kitabaka na kuwashinda, mwaka 829 alifanikiwa kuingia madarakani akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi silsila ya utawala wa Wasaxoni wa Magharibi.

Egbert

Katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Allamah Muhammad Iqbal Lahori mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu aliaga dunia huko Bara Hindi. Alizaliwa mwaka 1873 katika mji wa Sialkot kwenye jimbo la Punjab. Baada ya kumaliza masomo ya awali na ya juu na kupata shahada ya uzamili, Allamah Muhammad Iqbal Lahori alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne. Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya sekondari. Baada ya kurejea India, Iqbal Lahori alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi. Mwanafalsafa huyo anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi na waasisi wa Pakistan huru.

Muhammad Iqbal Lahori

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita aliaga dunia Sohrab Sepehri malenga na mchoraji mashuhuri wa Kiirani. Sohrab alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsiya katika mji wa Kashan katikati mwa Iran. Awali malenga huyo wa Kiirani alianza kufundisha na baada ya hapo alijiunga na taaluma ya sanaa. Vilevile alikuwa na kipaji kikubwa katika masuala ya uchoraji. Kazi za malenga na mchoraji huyo wa Kiirani zilimpatia tuzo na zawadi nyingi katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya Iran. Shairi lake la kwanza alilitunga mwaka 1330 Hijria Shamsiya na kulipa jina la The Death of Colours.

Sohrab Sepehri

Na leo tarehe Mosi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Saadi Shirazi alizaliwa karibu mwaka 606 Hijria Qamariya katika familia ya kielimu kwenye mji wa Shiraz ulioko kusini mwa Iran na baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa, akiwa kijana Saadi Shirazi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na katika maeneo mengine. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo za mashairi cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan. 

Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi