Apr 28, 2022 21:58 UTC
  • Ijumaa tarehe 29 Aprili 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 29 mwaka 2022.

 Miaka 883 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".

Siku kama ya leo miaka 333 iliyopita aliaga dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Allamah Majlisi aliandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa sala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Uislamu na Ahlul Bait zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Allamah Muhammad Baqir Majlisi

Miaka 168 iliyopita siku kama leo Henri Poincare mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa alizaliwa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi.

Henri Poincare

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Uislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kwa jina la Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo.

Mustafa Kamal Ataturk

Miaka 77 iliyopita katika siku kama ya leo majeshi ya Muungano yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi Waitifaki wa Ulaya vilifanya mashambulizi ya pande zote dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Musolini. Baada ya ushindi huo askari karibu milioni moja wa Ujerumani waliokuwa nchini Italia walijisalimisha kwa majeshi ya Waitifaki.

Leo, Ijumaa ya mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Siku kama hii ya leo miaka 43 iliyopita, yaani tarehe 13 Ramadhani mwaka 1399 hijria Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Imam aliitaja siku hiyo ya Quds kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu. Tangu wakati huo kila mwaka Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani huadhimishwa kwa kufanya maandamano makubwa ya Waislamu nchini Iran na maeneo mengine ya dunia dhidi ya utawala haramu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu. Tangazo hilo la Imam Khomeini liliungwa mkono na Waislamu kote duniani na lilidhihirisha kuwa, suala la ukombozi wa Quds Tukufu haliwezekani kwa kutumia njia ya kufanya mazungumzo na utawala ghasibu wa Israel unaoendelea kuwaua na kuwakandamiza wananchi wa Palestina.