Apr 29, 2022 22:43 UTC
  • Jumamosi, 30 Aprili, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 28 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1443 Hijria sawa na tarehe 30 Aprili 2022 Miladia.

Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawa na tarehe 30 Aprili, inafahamika kuwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi. Siku hii iliitwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuiita kwa majina mengine yasiyo na msingi Ghuba ya Uajemi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson. Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na ya kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya taifa ya Ghuba ya Uajemi. ***

Ghuba ya Uajemi

Siku kama ya leo miaka 1171 iliyopita aliaga dunia Abu Ma'ashar Balkhi mmoja wa wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya hadithi wa Kiirani. Alielekea Baghdad mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Katika zama zake, Abu Ma'ashar Balkhi alikuwa mnajimu mashuhuri wa Kiislamu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Mad'khal al-Kabir na al-Mawalid as-Saghirah. ***

Abu Ma'ashar Balkhi

Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani. Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mno mwanawe ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo alitabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78. ***

Carl Friedrich Gauss

Tarehe 30 Aprili mwaka 1945 dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa mafichoni chini ya ardhi baada na kufeli ndoto yake ya kutawala dunia nzima. Hitler alizaliwa mwaka 1889 nchini Austria na alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia katika safu za kwanza za askari wa Ujerumani. Adolf Hitler alianzisha chama cha National Socialist German Workers baada ya kuchanganya itikadi za kisoshalisti na mitazamo mikali ya utaifa. Na ulipotimia mwaka 1939 alianzisha Vita vya Pili vya Dunia. ***

Adolf Hitler

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita alifariki dunia malenga, mwandishi na msanii wa uchoraji wa zama hizi wa Iran, Ustadh Ismail Ashtiyani. Baada ya masomo ya msingi na upili, Ustadh Ashtiyani alijifunza sanaa ya kuchora kwa msanii mashuhuri wa zama hizo Kamalul Mulk. Mwaka 1307 Hijria Shamsia alishika wadhifa wa mkuu wa Chuo cha Sanaa cha Darul Funun. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na diwani ya mashairi, Kumbukumbu ya Ulaya na Historia ya Kamalul Mulk. ***

Ustadh Ismail Ashtiyani.

Tarehe 10 Ordibehesht miaka 43 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri. Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo. ***

Anwar Sadat

Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, operesheni kubwa ya Baytul-Muqaddas ilianza. Lengo la opesheni hiyo ya kijeshi lilikuwa ni kukomboa sehemu kubwa ya maeneo ya kusini mwa Iran yaliyokuwa chini ya udhibiti na uvamizi wa jeshi la chama cha Baath cha Iraq cha dikteta Saddam Hussein. Mji muhimu na wa kistratejia wa Khorramshahr ulikombolewa mwishoni mwa operesheni hiyo. Mji wa Khorramshahr unajulikana kama nembo ya muqawama na kusimama kidete vijana wa Kiirani mbele ya wavamizi wa Kibaathi. Jeshi la Baath la Iraq lilishindwa vibaya katika operesheni hiyo huku likipoteza wanajeshi wake waliouawa na wengine kutekwa nyara sambamba na silaha zake nyingi kuchukuliwa ngawira. Utawala wa dikteta Saddam ulipata pigo pia kimataifa.***

Operesheni kubwa ya Baytul Muqaddas