Alkhamisi tarehe 5 Mei 2022
Leo ni Akhamisi tarehe 3 Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 5 Mei mwaka 2022.
Leo tarehe 15 Ordebehesht Hijiria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Swaduq, msomi mashuhuri wa Kiislamu. Abu Ja'far Muhammad Ibn Ali ibn Babawayh maarufu kwa jina la Sheikh Swaduq alizaliwa katika ene9o la Qum nchini Iraq yapata mwaka 306 Hijiria katika familia ya wasomi. Akiwa kijana mdogo alianza kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu na kufanikiwa kukwea marhala za elimu kutoka kwa baba yake na maulama wengine wa zama zake. Baada ya hapo alifikia daraja za juu katika elimu, huku akifanya safari katika maeneo tofauti kwa ajili ya kusoma zaidi na kukusanya hadithi ambapo inaelezwa kuwa alipata kusoma kwa wasomi zaidi ya 200 wa zama zake. Baada ya kufanya safari mjini Baghdad, wasomi wa mji huo walivutiwa naye sana na wakapata kusoma kwake. Miongoni mwa wanafunzi wake ni pamoja na Sheikh Al-Mufid, Hassan Bin Muhammad Qumi, Alamul-Huda Sayyid Murtadha, na wengine wengi. Ameacha athari nyingi ambazo miongoni mwazo ni 'Man laa Yahdhuru al-Faqihi' chenye juzuu nne ambacho ni kati ya vitabu mashuhuri kwa Waislamu wa Shia na chenye hadithi 6000 na pia kitabu cha 'Madinatul-Ilm' chenye juzuu 10, 'Aamaal, Khiswaal', 'Uyuunu Akhbaar al-Ridha (as)' na 'Ilalu ash-Sharaaii'.
Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni. Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya. Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya.
Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu kwa ujumla na kusema: Kuanza harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia. Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu. Imam pia alieleza sababu za hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha umma.
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Bobby Sands mwanamapambano maarufu wa Ireland baada ya kukaa katika jela ya Uingereza kwa wiki kadhaa na kugoma kula chakula kwa muda wa siku 66 katika kupigania uhuru wa Ireland ya Kaskazini. Serikali ya kikoloni ya Uingereza ilikabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kufuatia kifo cha Bobby Sands na wanaharakati wenzake wa Ireland ambao waligoma kula chakula wakiwa katika jela za nchi hiyo.
Na tarehe 5 Mei imetangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirikisho la Kimataifa la Wakunga kuwa ni ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga. Siku hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza kuwa Siku ya Kimataifa ya Wakunga mwaka 1980 na kutangazwa rasmi mwaka 1992. Lengo la kuainishwa siku hii kuwaenzi wakunga na kazi ya ukunga, kuzidisha uelewa na kubadilishana maarifa na taarifa zinazohusiana na afya ya akina mama na watoto wachanga na vilevile kuonyesha umuhimu wa kazi za wakunga.
