Ijumaa tarehe 6 Mei mwaka 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 4 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Mei 2022.
Miaka 1092 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Muhammad bin Hassan Dar Qutni mmoja wa maulama na wataalamu wa lugha wa karne ya Nne Hijria. Dar Qutni alikuwa miongoni mwa maqari na wafasiri watajika wa Qu'rani Tukufu katika zama zake. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kuandika vitabu katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Muujamul Kabiir, al Maudhi'i fii Maanil Qur'an na al Manasik.
Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa Czechoslovakia, Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili na raia wa Austria. Akiwa na umri wa miaka minne alihamia mjini Vienna akiwa na wazazi wake. Aidha alipofikisha umri wa miaka saba alijiandikisha katika chuo kidogo cha udaktari ambapo akiwa na miaka 29 alitokea kuwa tabibu aliyebobea kutibu magonjwa ya akili. Baada ya kutibu wagonjwa kadhaa wenye matatizo hayo alipata uzoefu mkubwa suala ambalo lilimsukuma kufanya majaribio kadhaa katika uga huo. Daktari huyo alifanya utafiti na kutwalii matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa ajili hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis. Sigmund Freud alifariki dunia tarehe 23 Septemba 1939 akiwa na umri wa miaka 83 baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.
Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani, Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa.
Tarehe 6 Mei miaka 140 iliyopita mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch ilitangaza habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimefupisha umri wa zaidi ya watu bilioni moja wiki mbili kabla. Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka.
Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prf Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxy inayoshabihiana na Quinine. Prf Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika