May 09, 2022 02:25 UTC
  • Jumatatu tarehe 9 Mei 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 7 Mfungo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 9 Mwaka 2022.

Siku kama hii ya leo miaka 1440 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislamu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza, ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi kamili na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Siku kama ya leo miaka 369 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Isa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan.

Taj Mahal

Tarehe 9 Mei miaka 217 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.

Friedrich Von Schiller

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa.

Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 19 Ordibehesht mwaka 1306 Hijria Shamsia, sheria ya "Capitulation' ilifutwa na Bunge la Kitaifa la Iran. Kimsingi sheria hii ilikuwa na lengo la kuwapa kinga ya kutoshtakiwa raia wa kigeni waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Haki ya  'Capitulation' ilitumika mara ya kwanza nchini Iran baada ya mapatano ya Torkmanche ya mwaka 1206 wakati wa utawala wa Fath-Ali Shah ambapo Warusi walipata kinga hiyo na baada ya hapo serikali zingine za kigeni nazo ziliweza kupata haki hiyo ya raia wao kutoshtakiwa nchini Iran. Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa tena na bunge la kitaifa la Iran mwaka 1343 kwa lengo la kuwapa kinga Wamarekani. Imam Khomeini MA alipinga vikali sheria hiyo na utawala wa Shah ulikasirishwa sana na malalamiko hayo na ukachukua uamuzi wa kumbaidisha Imam nchini Uturuki. Hatimaye, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, sheria ya 'Capitulation' ilifutwa daima nchini Iran.

Capitulation

Siku kama hii ya leo miaka 50 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Shawwal 1393 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Shaarani mfasiri wa Qurani Tukufu inayojulikana kwa jina la 'Manhaj Swadiqiin', akiwa na umri wa miaka 73. Msomi huyo licha ya kubobea katika elimu za kidini alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama vile Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Licha ya kuonyesha uwezo wake katika tafsiri ya Qurani Tukufu ya Manhaj Swadiqiin chenye juzuu 10 aliacha athari ya kitabu cha Sharh Kifayatil Usul.

Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani