May 11, 2022 01:49 UTC
  • Jumanne tarehe 10 Mei 2022

Leo ni Jumanne tarehe 8 Shawwal 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Mei mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, yaani sawa na tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge.

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario. Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania. Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya nchi hiyo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco.

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Sayyid Jawad Mustafavi mwandishi, mhakiki na mhadhiri wa zama hizi wa kiirani alifariki dunia.  Awali alisoma masomo ya kidini sambamba na kufanya utafiti katika fani mbalimbali katika uwanja huo. Jawad Mustafavi alibobea mno katika elimu za kidini. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha elimu za dini mjini Mash'had. Aidha msomi huyo hakuwa nyuma katika uga wa kualifu vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Kashif na Miftaful al-Wasail.

Dakta Sayyid Jawad Mustafavi

Tarehe 10 Mei miaka 28 iliyopita yaani tarehe 10 Mei 1994, Nelson Rolihlahla Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya zaidi ya karne tatu za utawala wa makaburu wachache nchini humo. Chama cha African National Congress (ANC) kilijipatia viti 252 kati ya jumla ya viti 400 vya Bunge la Afrika Kusini, kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na wa kihistoria nchini humo. Baada ya kuchaguliwa, Rais Mandela alimteua Thabo Mbeki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na FW de Klerk kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Afrika Kusini.

Nelson Rolihlahla Mandela