May 11, 2022 02:03 UTC
  • Leo ni Jumatano tarehe 11 Mei 2022

Leo ni Jumatano tarehe 9 Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 11 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1333 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Sirin mpokezi wa hadithi na faqihi mashuhuri wa karne ya pili Hijria aliaga dunia. Ibn Sirin alizaliwa Basra kusini mwa Iraq. Msomi huyo wa Kiislamu alitoa umuhimu mkubwa kwa hadithi za Mtume Muhammad SAW na alikuwa mahiri katika kuhifadhi na kunukuu hadithi. Alikutana na masahaba 30 wa Mtume Muhammad (saw). Ibn Sirin ameacha vitabu na makala nyingi zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali. Kutokana na hali hiyo wataalamu wengi wa hadithi wanatilia maanani sana hadithi zilizopokelewa na Ibn Sirin. 

Hii leo vitabu mbalimbali na kwa lugha tofauti vimeandikwa kutoka kwa msomi huyo. Ibn Sirin anafahamika pia kwa uhodari wake wa kufasiri ndoto.

Siku kama ya leo miaka 326 iliyopita, yaani tarehe 11 Mei mwaka 1696 Miladia, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa.

ean de La Bruyère

Tarehe kama ya leo miaka 158 iliyopita alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21 Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960.

Ethel Lilian Voynich

Siku kama ya leo, miaka 155 iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867 Miladia, iliundwa nchi ya magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo imezungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa.

Bendera ya Luxembourg

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa mwasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989.

Salvador Felipe Dali

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho cha kwanza cha matangazo ya televisheni kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa  wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha.

Paul Gottlieb Nipkow

Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya pamoja ya Ufaransa na Uingereza yaliwasili nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. Hatua hiyo ya Ufaransa na Uingereza ya kuiunga mkono Ubelgiji ilikuwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwako baina ya nchi hizo. Licha ya kuweko muungano huo wa kijeshi, vikosi vya Ujerumani ya Kinazi mbali na kuyashinda majeshi ya Ubelgiji vilivishinda pia vikosi vya  pamoja vya Uingereza na Ufaransa na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi hiyo.

Vita vya Pili vya Dunia