Jumamosi, Juni 4, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 4 Juni mwaka 2016 Miladia, sawa na tarehe 28 Shaaban mwaka 1437 Hijria.
Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 15 Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano kulalamikia hatua ya askari vibaraka wa Shah ya kumkamata Imam Khomeini MA. Imam Ruhullah Khomeini (MA) alikamatwa baada ya kutoa hotuba ya kihistoria dhidi ya madola ya kibeberu na kiistikbari katika Chuo cha Kidini cha Fayziya mjini Qum. Kukamatwa kwa Imam Khomeini MA kulizusha ghadhabu miongoni mwa wananchi Waislamu wa Iran na kuwapelekea wafanye maandamano yasiyokuwa na kikomo. Idadi kubwa ya wananchi waliuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika maandamano hayo. Mwamko wa Khordad 15 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, uliandaa mazingira ya kufanyika Mapinduzi dhidi ya utawala wa kidekteta wa Pahlavi. Kuanzia siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran chini ya miongozo ya Imam Khomeini MA waliendelea na maandamano hadi terehe 22 Bahman mwaka 1357, siku ambayo harakati zao za kimapinduzi zilipata ushindi.
<<<<<>>>>>>>>>>
Tarehe 4 Juni miaka 1982 iliyopita, kufuatia dhuluma na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Lebanon na Palestina, Umoja wa Mataifa ulitagaza terehe ya leo kuwa Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia, Wahanga wa Uvamizi na Ghasia. Umoja huo ulitenga siku hii kwa ajili ya kushutumu mateso, dhiki, ukandamizaji wa kimwili na kisaikolojia wanaopitia watoto kutokana na ghasia na machafuko katika sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watoto laki 2 na elfu 50 wanatumika kama askari kote duniani, aghalabu yao wakiwa wahanga wa utekaji nyara na baadhi wakilazimishwa au wakilazimika kujiunga na vikosi vya waasi kutokana na ukata na umaskini. Zaidi ya asilimia 50 ya wakimbizi milioni 50 kote duniani ni watoto. Kati ya wakimbizi milioni 22 ambao wanapatiwa hifadhi na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHRC katika pembe mbali mbali za dunia, milioni 10 ni watoto wenye umri usiozidi miaka 18.
<<<<<<<<<<><>>>>>>>>
Siku kama ya leo, miaka 807 iliyopita, yaani tarehe 28 Shaaban mwaka 630 Hijria Qamaria, alifariki dunia mwanahistoria maarufu wa Kiislamu na mpokezi wa Hidithi kwa jina la Ibn Haajib. Ibn Haajib alizaliwa mwaka 593 Hijria mjini Damascus nchini Syria. Msomi huyo alisafiri katika miji mbali mbali ili kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wa enzi zake. Kutokana na ueledi na ujuzi wake katika elimu ya Hadith, mwanahistoria huyo ameandika vitabu kadhaa ambapo vitatu miongoni mwavyo vimechapishwa.
<<<<<<<<<<<<<<>>>>>>>>>>
Na siku kama ya leo, miaka 126 iliyopita, sawa na tarehe 28 Shabaan mwaka 1311 Hijria, Mullah Husseingholi Hamadani, msomi mashuhuri wa somo la Akhlaqi wa Iran aliaga dunia. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 1238 Hijria na kujipatia elimu ya tabia njema na maadili bora kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Kwa mujibu wa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu kama vile Shahidi Mortaza Motahhari msomi, mwanafilosofia na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu, darsa za alkhlaki za Mullah Husseingholi Hamadani katika hauza ya mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq zilikuwa ni za malezi zaidi kuliko masuala ya kielimu.