Jun 05, 2022 23:26 UTC
  • Jumatatu, 06 Juni, 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 6 Mfunguo Pili Dhul Qaadah, 1443 Hijria, sawa na tarehe 6 Juni 2022

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita mwili mtoharifu wa hayati Imam Khomeini (MA) ulisindikizwa na kuzikwa mjini Tehran na umati wa mamilioni ya wapenzi wake waliojawa na huzuni na majonzi mengi. Zaidi ya watu milioni kumi kutoka miji mbalimbali ya Iran na nchi kadhaa walishiriki katika maziko ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hali muhimu zaidi ya kipekee kuhusu maziko ya Imam Khomeini, ambaye aliutumia umri wake wote kupigania ukombozi na heshima ya wananchi, ni kuonekana maziko hayo kuwa ni suala la umma. Siku hiyo mwili wa Imam Khomeini, ambao siku ya kabla yake uliwekwa kwenye uwanja mkuu wa kusalia wa mjini Tehran kwa ajili ya kuagwa na wananchi, ulisindikizwa kutoka hapo hadi kwenye eneo la makaburi la Behesht Zahra kusini mwa Tehran, kisha ukazikwa kando ya makumi ya maelfu ya makaburi ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa Vita vya Kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Leo hii haram ya kiongozi huyo mkubwa pamoja na maziara safi ya makumi ya maelfu ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kituo cha kuzuru wapenzi wake na makutano ya kujumuika wapenzi wa Wilaya na Mapinduzi ya Kiislamu.

Haram ya Imam Khomeini (MA)

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, tarehe 6 Juni 1982, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel liliushambulia tena na kuukalia kwa mabavu mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Wakati wa hujuma na uvamizi huo wa ardhi ya Lebanon, askari wa utawala haramu wa Israel waliiteketeza miundomsingi ya kiuchumi, viwanda na miji ya nchi hiyo na kufanya jinai nyingi sana. Septemba mwaka huohuo yalifanyika mauaji ya kutisha ya halaiki ya wakimbizi Wapalestina katika kambi mbili za Sabra na Shatila karibu na Beirut. Lakini licha ya yote hayo wanamapambano Waislamu wa Lebanon waliendeleza muqawama na mapambano ya kukabiliana na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na kuanza kuwarejesha nyuma hatua kwa hatua; na baada ya kuliendesha mchakamchaka jeshi la utawala huo haramu na vibaraka wake wa kusini mwa Lebanon kwa vipigo vizito kadhaa, hatimaye mnamo mwezi Mei mwaka 2000, Wazayuni walilazimika kukimbia kimadhila katika maeneo ya ardhi ya Lebanon waliyokuwa wakiyakalia.

Beirut ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni 1982

Miaka 129 iliyopita, mnamo tarehe 6 Dhul-Qaadah 1314 hijria, aliaga dunia Mirza Abul Hassan Jalwa, Hakim, Arif na mwalimu mkubwa wa akhlaqi. Mirza Abul Hassan Jalwa alizaliwa mwaka 1238 Hijria katika mji wa Ahmadabad nchini India. Nasaba yake ya baada ya vizazi 30 inaishia kwa Imam Hassan Al-Mujtaba (AS). Katika umri wa utotoni Mirza Abul Hassan Jalwa alielekea Esfahan Iran pamoja na familia yake; na huko ndiko alikosomea na kuleleka kimaanwi. Mwaka 1273 alielekea Tehran, ambapo kwa zaidi ya miaka 40 alifanya kazi ya kusomesha hikma, falsafa na hisabati katika chuo cha Daarush-Shifaa. Miongoni mwa wanafunzi wake maarufu ni Mirza Tahir Tankabani, Ayatullah Muhammad Ali Shah Abadi, Sayyid Hussein Badkubei, Mulla Muhammad Amoli, Jahangir Khan Qashqai na Allama Tabatabai. Mirza Abul Hassan Jalwa ameacha athari nyingi za vitabu na maandiko, miongoni mwao ni Shifaa na Asfar na Ithbatul-Harakatil-Jawhariyyah. Hatimaye hakim na arif huyo mkubwa aliaga dunia siku ya Ijumaa usiku, tarehe 6 Dhul Qaadah mjini Tehran akiwa na umri wa miaka 76.

Mirza Abul Hassan Jalwa

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa kabisa la makalasinga liitwalo Hekalu la Dhahabu katika mji wa Amritsar kwenye jimbo la Punjab magharibi mwa nchi hiyo na kuwaua wapiganaji wa msituni wa Kikalasinga wapatao elfu moja. Kwa mujibu wa serikali ya India, makalasinga wanaopigania kujitenga walikuwa wamekusanya silaha nyingi ndani ya hekalu hilo wakiwa na lengo la kuzitumia dhidi ya serikali kuu kuendeshea mapambano na kujitangazia uhuru, kisha kuunda nchi itakayoitwa Khalistan itakayotawaliwa na makalasinga. Hujuma na shambulio hilo la jeshi la India dhidi ya hekalu la dhahabu lilizima mpango huo na kuwadhooifisha makalasinga waliokuwa wakipigania kujitenga. Lakini nao pia waliamua kulipiza kisasi cha shambulio hilo lililotekelezwa kwa amri ya waziri mkuu wa wakati huo wa India Indira Gandhi walipomuua kiongozi huyo tarehe 31 Oktoba mwaka huohuo wa 1984 kupitia walinzi wake wawili ambao walikuwa makalasinga.

Hekalu la dhahabu

Na tarehe 6 Juni ni Siku Taifa ya Sweden.

Falsafa ya kupewa siku hii jina hilo la Siku ya Taifa ya Sweden ni tukio la kutungwa katiba ya kwanza ya nchi hiyo miaka 206 iliyopita katika siku kama ya leo. Sweden ni nchi yenye ukubwa wa kilomitamraba 449,964; iko kaskazini ya Ulaya kando ya Bahari ya Baltik na imepakana na nchi za Norway, Finland na Denmark. Nchi hiyo ina idadi ya watu milioni tisa ambao karibu asilimia 90 miongoni mwao wana asili ya Sweden na wanafuata madhehebu ya Protestanti. Lugha ya taifa nchi hiyo ni Kisweden na mji mkuu wake ni Stockholm. Mfumo wa kisiasa wa Sweden ni Ufalme wa Kikatiba ambapo cheo cha ufalme ni cha heshima tu. Sweden inatambuliwa kuwa moja ya nchi tajiri zaidi na zilizoendelea zaidi duniani.

Bendera ya Sweden