Jumatano, Juni 8, 2022
Leo ni Jumatano mwezi 8 Mfunguo Pili Dhulqaad 1443 Hijria, sawa na tarehe 8 Juni 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1095 yaani tarehe mwezi 8 Mfunguo Pili Dhulqaad mwaka 348 Hijria, alifarikia dunia mwandishi Muislamu Abul Hasan Ali bin Zubair Kufi, mjini Baghdad, Iraq. Alianza masomo yake kutoka kwa baba yake. Baada ya kufarikia dunia baba yake, ibin Zubair alitumia mali aliyoirithi kutoka kwa baba yake, kutafuta elimu na maarifa, kusaidia kujenga maktaba na pia kusaidia masuala ya elimu na utafiti. Mwanachuoni huyo alisaidia sana mapinduzi ya utungaji na utunzaji wa vitabu vya elimu tofauti. Wanachuoni wakubwa wa zama zake walitumia kazi zake akiwemo Ibn Nadhir, mwanahistoria maarufu wa zama zake.
Tarehe 8 Juni miaka 167 iliyopita, Lisbon mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi arubaini elfu (40,000) wa mji huo walipoteza maisha yao na thuluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngarawa (ngalawa) nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi ya ardhi kuwahi kuikumba Ureno.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, shirika la kijasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa. Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa unawaka taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii.