Jun 08, 2022 21:47 UTC
  • Alkhamisi, Juni 9, 2022

Leo ni Alkhamisi mwezi 9 Mfunguo Pili Dhulqaad, 1443 Hijiria inayosadifiana na 9 Juni 2022 Milaadia.

Tarehe 29 Dhilqaada miaka 1083 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya hadithi za Mtume SAW. Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya kufanya utafiti na uchunguzi wa miaka 33. Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya hadithi kwa majina ya al Muujamul Kabiir, al Muujamul Ausat na al Muujamu Swaghir.

Abul Qasim Tabarani

 

Siku kama ya leo miaka 1954 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Juni mwaka wa 68 Milaadia, Mfalme Nero Claudius Caesar mtawala katili na aliyemwaga damu nyingi wa Rome alijiua, baada ya kuishi kwa miaka 31 na kutawala kwa maiaka 14. Si vibaya kuashiria hapa kwamba Nero alitangazwa kuwa mwana kamili wa mjomba wake Mfalme Claudius aliyekuwa mtawala wa kwanza wa Rome. Lakini Nero alimpa sumu mfalme huyo na kuchukua nafasi yake baada ya kufa. Mfalme huyo katili na wa mwisho wa Rome, wakati wa utawala wake aliwaua watu wengi wa familia yake akiwemo mama yake, mkewe, kaka yake na ndugu zake wengine. Pia aliwaua wananchi wake wengi. Aliwaua kwa umati Wakiristo pamoja na kuuchoma moto mji wa Rome.

Nero Claudius Caesar

 

Miaka 137 iliyopita muwafaka na leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika. Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalikuwa sehemu bora kwa watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa." Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960.

Togo

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisaabishwa na jeshi la siri la Ufaransa.

Jengo la hivi sasa la Maktaba ya Taifa ya Algeria

 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa Tabrizi huko kaskazini mwa Iran mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea  Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa, Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari katika elimu za Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na malezi na kutoa elimu kwa wanafunzi. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Uhusiano wa Kimaanawi Baina ya Roho na Sauti. 

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai