Jumamosi, 11 Juni, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1443 Hijria sawa na tarehe 11 Juni 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1295 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume (as). ***

Miaka 1107 iliyopita katika sikku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 11 Dhul Qaad 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati zake za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa Madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usulul Fiqh. ***
Katika siku kama ya leo miaka 450 iliyopita sawa na tarehe 11 Juni mwaka 1572, alizaliwa Benjamin Jonson mshairi na mwandishi wa filamu wa Uingereza. Jonson kwa muda mrefu alikuwa mcheza tamthilia na alikuwa rafiki wa Shakespare mwandishi maarufu wa Uingereza, ambapo urafiki wao ulikuwa na athari kubwa katika kukamilisha fasihi ya mshairi huyo. Baadhi ya athari zilizoachwa na Benjamin Jonson ni Mwanamke Aliyezimwa' pamoja na Historia ya Dunia. Malenga huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1637. ***
Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Haitham na Qutbuddin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen. ***

Na miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhammad Khazaeli, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia Vipofu ya Iran. Khazaeli alipokuwa mtoto alipoteza nguvu ya kuona kutokana na ugonjwa wa ndui, na alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Dakta huyo kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Khazaeli alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali. Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la kitaifa la kuwahudumia vipofu na Jumuiya ya Kimataifa ya Vipofu. ***