Jumatatu, Juni 13, 2022
Leo ni Jumatatu mwezi 13 Mfunguo Pili Dhulqaad 1443 Hijria, sawa na tarehe 13 Juni 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 677 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Muhammad Razi. Razi alizaliwa katika eneo la Varamin kwenye viunga vya mji wa Rey na alipata umashuhuri kwa jina la Razi kwa kuwa alikulia katika mji huo. Qutbuddin Muhammad Razi alikuwa mwanafunzi mkubwa wa Allamah Hilli. Kwa kipindi fulani aliwatumikia Sultan Abu Said na waziri wake Khaja Ghiyathuddin Muhammad na aliandika viwili vya 'Sharhu al-Shamsiyyah' na 'Sharhul Matwaali' kwa jina la waziri huyo.' Baada ya kufariki dunia Sultan Abu Said, Qutbuddin Muhammad Razi alielekea Sham na alifariki dunia mjini Damascus.

Siku kama ya leo miaka 415 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Isterabadi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na elimu ya theolojia. Ayatullah Mirza Muhammad Bin Ali Bin Ibrahim Isterabadi alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Awali alikuwa akiiishi mjini Najaf, Iraq na baadaye alielekea Makkah na kufanya makazi mjini hapo. Isterabadi ni kati ya watu wanaoelezwa kuwa waliopata sharafu ya kukutana na Imam wa zama (af). Msomi huyo aliandika vitabu juu ya wapokezi wa hadithi kikiwemo kitabu cha 'Tawdhihul-Maqaal' 'Talkhisul-Aqwaal' na 'Manhajul-Maqaal.' Vitabu hivyo vinatambuliwa kuwa vitabu muhimu na chemchemi ya elimu ya wapokezi wa hadithi.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.