Hassanain katika Aya ya Tat'hir 2
Assalaam Alaikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Terhran. Karibuni katika sehemu hii ya 6 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Aya na Hadithi ambayo kwa leo pia itaendelea kuzungumzia sehemu ya pili ya Aya ya Tat'hir ambayo inasema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara.
Mamia ya vyanzo na marejeo ya Hadithi za Kishia na za Kisuni, yote yanathibitisha kwamba Aya hii iliwateremkia Ahlu Kisaa yaani Watu wa Kisaa ambao ni Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein ambao wote ni Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) kwa kuwa hakuna watu wengine waliokusudiwa na Aya hiyo tukufu kama tulivyoona katika kipindi kilichopita. Aya hii ndio moja ya sababu za kutengewa watukufu hawa istilahi hii ya Qur'ani ya Tat'hir, la sivyo, kama ingekuwa inawajumuisha watu wengine wasiokuwa hao tungesikia madai hayo kutoka kwa watu hao.
As-Shablanji as-Shafi' ameandika katika kitabu chake cha Nur al-Abswar fi Manaqib Aali Bait an-Nabiy al-Mukhtar, kwamba: Imepokelewa kupitia njia kadhaa sahihi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Mungu (saw), alikuja huku akiwa ameandamana na Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na kisha akawafunika shuka na kusoma Aya inayosema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara. Baada ya kusoma Aya hiyo alisema: 'Ewe Mwenyezi Mungu hawa ndio Ahlu Bait wangu, hivyo waondolee uchafu na uwatakase baarabara.' Na katika Riwaya ya Ummu Salama alisema: Nilifungua shuka ili nami nipate kuingia humo pamoja nao, lakini Mtume aliivuta kutoka mikononi mwangu, nikasema: Je, na mimi niko pamoja nanyi ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Hakika wewe ni mmoja wa wake za Mtume na uko kwenye heri.'
**********
Ndugu wasikilizaji, idadi kubwa ya masahaba wa Mtume (saw) na wafuasi wao pamoja na wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wameafikiana kwamba Aya tukufu ya Tat'hir iliteremshwa kuwahusu watukufu watano watoharifu ambao wote ni Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Kwa mfano, Tabari ananukuu katika kitabu chake cha Jamiu al-Bayaan Riwaya ambayo imepokelewa na Abu Said al-Khidri kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: Aya hii iliteremka kunihusu mimi, Ali, Hassan, Hussein na Fatwimah.' Na suala hilo limesisitizwa pia na Ibn Kathir, at-Tabrasi, as-Shaukani, Hakim Naishaburi as-Shafii', Ibn Hajar al-Haithami na wengine wengi. Mtume (saw) alisisitiza kivitendo kwamba Aya hiyo ya Tat'hir iliteremka kuwakusudia Ahlu Bait wake (as) ambapo kila mara wakati wa swala ulipofika yaani mara tano kwa siku, alikuwa akipita nyumbani kwa Ali na Fatwimah (as) na kushika mlango wao kuwaita kwenye swala huku Waislamu wakimsikia akisema: Salamu, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu! Swala! Mwenyezi Mungu akurehemuni! Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara.' Imepokelewa kwamba Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akifanya hivyo maisha yake yote alipokuwa mjini Madina hadi alipoaga dunia. Abu Hamra na Ibn Abbas walimwona akifanya hivyo kwa muda wa meizi tisa, Anas bin Malik miezi sita na Abu Burzah miezi saba.
Baada ya hapo wapenzi wasikilizaji, tunapasa kujua maana ya utakasaji uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika Aya hii ya Tat'hir ambao ameubana katika Ahlu Bait wa Mtume Muhammad al-Mustafa (saw) peke yao, bila ya kuhusishwa watu wengine.
**********
Ndugu wasikilizaji, inasemekana kuwa uchafu unaokusudiwa hapa ni dhambi inayotokana na kuacha maamrisho, na kutenda makatazo ya Mwenyezi Mungu. Vilevile uchafu huo umearifishwa kuwa ni shaka, mabaya, maasi na kutenda matendo ya kishetani ambayo Mwenyezi Mungu hayaridhii. Uchafu umetumika hapa kwa maana ya dhambi kama ambavyo takwa imetumika kumaanisha usafi na utoharifu. Hivyo Aya ya Tat'hir imetumika kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu ametaka kuwaondolea Ahlul Bait (as) yaani Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) kila aina ya uchafu, maasi na dhambi na kuwavisha vazi la utukufu, utakatifu na utoharifu. Tusisahau hapa wapenzi wasikilizaji kwamba utoharifu unakusanya usafi wa akili, roho, mwili, nafsi, dhamira, itikadi, maadili na mambo mengine mengi. Kwa ufupi ni kuwa jambo hilo linahitajia isma na kinga ya kutofanya dhambi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe. Kwa msingi huo ni wazi kuwa Aya hii ilikusudia kusisitiza na kuzungumzia isma ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) ambao ni Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as). Jambo hilo linathibitishwa wazi na Riwaya ambayo imenukuliwa na Sheikh Sulaiman al-Qunduzi katika kitabu chake kinachoitwa Yanabiul Mawadda na ambayo imepokelewa kupitia Asbagh bin Nabata kupitia Abdullah bin Abbas kwamba alisema: 'Nilimsikia Mtume (saw) akisema: Mimi na Ali, na Hassan na Hussein na wengine tisa kutoka katika kizazi cha Hussein ni watoharifu na maasumu.' Na Sheikh al-Hamwayni al-Juwayni as-Shafii pia ameinukuu Riwaya hii katika kitabu chake cha Faraid as-Simtain fi Fadhail al-Murtadha wal Batul wa Sibtain. Je, kuna makusudio na maana nyingine ya Aya hii?! Ndio kuna maana nyingine nyingi tu lakini kwa bahati mabaya wakati hauturuhusu kuzizungumzia sote katika kipindi hiki kifupi. Hata hivyo, tunaashiria hapa moja ya maana hizo muhimu nayo ni uzingatiaji mkubwa na maalumu aliouonyesha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Ahlul Bait wa Mtume wake na kusisitiza juu ya utoharifu na utakatifu wao ambao unawaweka mbali na kila aina ya uchafu na dhambi. Wakati huohuo amewakutanisha watukufu hao na mbora wa viumbe wake Muhammad al-Mustafa (saw) katika fadhila na sifa zake tukufu. Shaikh as-Shablanji as-Shafii' ameashiria suala hilo katika kitabu chake cha Nur al-Abswar kwa kusema: Fakhr ar-Razi amesema kwamba Ahlu Bait wa Mtume (saw) walikuwa sawa naye katika mambo matano: Kumswalia yeye Mtume na wao (Ahlul Bait) kwa pamoja kwenye Tashahud, katika kuwatumia salamu, yaani 'Salaamun ala Aal Yasin', katika utoharifu, yaani Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara, katika kuharamishiwa sadaka na katika mahaba (kuwapenda), kupitia Aya inayosema: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika ndugu (Ahlul Bait).
Na kwa hayo ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili. Kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.