Jul 23, 2022 21:47 UTC
  • Jumapili tarehe 24 Julai 2022

Leo ni Jumapili tarehe 24 Dhulhija 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Julai 2022.

Siku kama ya leo miaka 1434 kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).

Siku kama ya leo miaka 239 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia. Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.

Simón Bolívar

Miaka 220 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.

Alexandre Dumas

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo.

Miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo. Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi.

Bandari ya Hamburg

Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini na vyombo vya usalama vya utawala wa Shah, maulamaa kadhaa na marajii kutoka Qum na Mash'had na miji mingine ya Iran walifunga safari na kuelekea Tehran. Mbali na kuandika barua wakithibitisha daraja ya Umarjaa ya Imam Khomeini walitoa wito wa kuachiliwa huru mwanazuoni huyo. Hatua hiyo sambamba na kuendelea upinzani wa wananchi dhidi ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kuliulazimisha utawala wa Shah kumhamisha kiongozi huyo kutoka jela na kumpeleka katika nyumba moja ili kuwatuliza maulama na wananchi hao. Siasa hizo za kutuliza mambo hazikuwa na taathira na kwa msingi huo utawala wa Shah ukiwa na lengo la kuweka pengo baina ya Imam Khomeini na wafuasi wake, uliamua kumbaidishia mwanazuoni huo nchini Uturuki na mwaka mmoja baadaye nchini Iraq.