Jun 06, 2016 22:55 UTC
  • Jumanne, Juni 7, 2016

Leo ni Jumanne, tarehe Mosi Ramadhan mwaka 1437 Hijria, inayosadifiana na Juni 7 mwaka 2016 Miladia.

Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehema na baraka za kiroho. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SW anasema: ((Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.))Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa Imam Hassan AS ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Aidha siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za kimaanawi za mwezi huu na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha Wake.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Siku kama hii ya leo miaka 135 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na kusababisha Chile kuishambulia kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo, na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru, ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Siku kama hii ya leo miaka 166 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni mwaka 1848 alizaliwa Paul Gauguin mchoraji mashuhuri wa Kifaransa. Gauguin alizaliwa Ufaransa na kisha kumuoa mwalimu aliyekuwa mahiri katika fani ya uchoraji, na kusababisha Gauguin kuvutiwa na sanaa hiyo iliyomuwezesha kuacha athari zake za sanaa ya uchoraji katika kisiwa cha Tahiti, kilichoko kusini mwa Bahari ya Pacific. Gauguin aliishi kwenye kisiwa hicho hadi mwisho wa umri wake mwaka 1903, kwa kuchora picha zinazoakisi mandhari mbalimbali.