Jun 11, 2016 05:07 UTC
  • Jumamosi, Juni 11, 2016

Leo ni Jumamosi, tarehe 5 Ramadhani mwaka 1437 Hijria, sawa na tarehe 11 Juni mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 791 iliyopita, sawa na tarehe 5 Ramadhani mwaka 646 Hijria Qamaria, aliaga dunia Afdhaluddin Abu-Abdullah Tabib Khunji, mtoto wa Abdulmalik Khunji, msomi na mwanafikra wa Kiislamu wa karne ya 7 Hijria Qamaria. Tabib Khunji alizaliwa mwaka 590 Hijria Qamaria katika mji wa Khunj, kaskazini magharibi mwa Iran na kuanza masomo yake ya msingi. Tabib Khunji alikuwa mtu wa busara, maarifa na alijifunza elimu ya tiba na masomo mengine ya kidini kama Fiqhi na Hadith. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Kashful Asrar” na “Ghawaamithul Afkaar fi Mantik".

XXXXXXXXXXXXXX

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita mwafaka na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Inafaa kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo husababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Hisham na Qutbudin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

XXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita, alifariki dunia Hussein bin Muhammad Swaleh Khalidi, mwanazuoni mkubwa wa karne ya 13 Hijiria. Alizaliwa huko Baitul Muqaddas na akiwa katika mji huo alianza kujifunza elimu mbalimbali za zama hizo. Khalidi alikuwa mwanazuoni mwenye basira, mwandishi aliyetabahari na pia alisifika kwa hati nzuri. Hassan bin Muhammad Saleh Khalidi vilevile alikuwa na kipaji cha kusoma vizuri mashairi hasa ya Kiarabu. Mwanazuoni huyo ameandika na kuacha nyuma vitabu kadhaa.