Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (53)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo mna karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti, mmoja wa wasomi na wanazuoni watajika aliyeishi katika karne ya 13 Hijria ambaye anajulikana katika jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa lakabu ya Hujjatul Islam Mutlaq.
Tulisema kuwa, Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti alizaliwa katika kijiji cha Chirza katika mkoa wa Zanjan nchini Iran. Baba yake alikuwa msomi na mwanazuoni wa kuchanganyika na watu na ni miongoni mwa wajukuu wa Imam wa saba wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Tulibainisha jinsi alivyokuwa mchamungu ambapo, wakati wa Swala, mwili wake ulikuwa ukitetemeka sana kwa hofu ya Mwenyezi Mungu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 53 ya mfululizo huu kitatupia jicho maisha ya Mirza Masih Mujtahid mwenye fatuwa mashuhuri ya Sharaf yaani heshima ambayo ilikuwa na nafasi muhimu katika matukio ya kijamii na kisiasa katika zama zake Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mirza Masih Mujtahid alizaliwa 1193 Hijria katika mji wa kijani kibichi na wenye mandhari nzuri wa Asterabad nchini Iran, mji ambao leo unajulikana kwa jina la Gorgan. Baba yake Kadhi Saeed Asterabad alitambulika kama mtu mwenye fadhila na mchamungu. Licha ya kuwa aliishi katika zama zilizokuwa na vurugu na machafuko, lakini alikuwa akifanya hima na idili kuhakikisha kwamba anaandaa mazingira mazuri ndani ya nyumba ambayo yatawafanya watoto kukua na kuleleka katika anga ya uchangamfu, utulivu na kushikamana na dini. Akitegemea maarifa na utamaduni wa Ahlul-Beiti (as) na itikadi za dini, aliandaa ratiba na mipango ya kueleweka kwa ajili ya kuwalea watoto wake ambapo wakiwa na umri wa miaka 7 aliwashajiisha mno kutekeleza ibada ya Swala huku akiwafundisha maadili mema ya Kiislamu.
Baada ya Masih Mujtahid kukamilisha masomo yake ya awali na ya msingi kwa baba yake, alianza kuhuhudhuria masomo katika Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini) katika mji aliozaliwa wa Asterabad. Baadaye alihajiri na kuelekea katika mji wa Qum Iran ambao katika zama hizo ulikuwa moja ya vituo vikubwa na muhimu vya kielimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Akiwa huko alisoma elimu mbalimbali kama fikihi, Usuli, hadithi na kadhalika kwa walimu watajika wa karne ya 13 kama Mirza Qumi. Kwa muda mfupi tu, Mirza Masih Mujtahid alichomoza na kuwa mmoja wa wanafunzi mahiri na stadi wa mwalimu huyo.
Baadhi wanasema kuwa, aliondokea kuwa mwanafunzi asiye na mithili wa Mirza Qumi. Baada ya kufanikiwa kufikia daraja ya Ijtihadi, Mirza Masihi Mujtahidi aligura na kuelekea katika mji wa Tehran. Alimu huyu ambaye alikuwa mchamungu na mtu aliyeipa mgongo dunia, baada ya kuwasili katika mji wa Tehran alitosheka na kuswalisha Swala ya Jamaa katika Msikiti wa Jamia sambamba na kueneza mafundisho ya fikihi na kujibu maswali ya watu na mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiwatatiza. Alikuwa akifuatilia kwa karibu mno na kutathmini hali ya watu wasiojiweza na kufanya idili na hima kubwa ya kuyapatia ufumbuzi matatizo yao.
Nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, alifanya kila aliloweza kwa ajili ya kuichunga jamii ya Waislamu na alipokuwa akiona mahali fulani kuna mambo yasiyofaa yanafanyika, au sheria za Kiislamu zinapuuzwa basi hakuwa akikaa na kuweka mikono nyuma bali alikuwa akiinuka na kufanya kila awezalo kuhakikisha kwamba, analeta mabadiliko na mageuzi katika jambo hilo. Sifa hiyo sambamba na kujipamba kwake na uchajimungu, maadili mema, bashasha na tabasamu kwa watu, unyenyekevu na usafi wa nafsi ni mambo ambayo yaliwafanya watu katika jamii wamthamini na kumkubali sana na hatua kwa hatua akaanza kuondokea kuwa mujtahidi mashuhuri zaidi mjini Tehran katika zama hizo.
Mirza Masih Mujitahid aliishi katika zama ambazo kutokana na kutokuweko viongozi stahiki na kujitokeza udhaifu katika utawala sambamba na hitilafu baina ya wanamfalme bila kusahau kujihusisha na starehe mfalme Fat'h Ali Shah Qajar, Iran ilikuwa imekumbwa na uporaji, hujuma na uvamizi uliokuwa ukifanywa na maajinabi. Warusi walitumia vibaya udhaifu huo na hitilafu baina ya wanamfalme wa Iran ambapo kufuatia hujuma na mashambulio yao mtawalia, walifanikiwa kuunganisha na utawala wao sehemu ya ardhi ya Iran na kulitwisha taifa hili mikataba ya fedheha na mibaya kama mkataba wa Turkmenchay (Treaty of Turkmenchay) ambao ulitiwa saini baina ya utawala wa Russia na ufalme wa Qajar. Mkataba huo ulipelekea sehemu kubwa ya ardhi ya Iran kuunganishwa na Russia. Mirza Masih Mujtahid kama walivyo Maulamaa wengine stahiki na wenye ghera hakuridhishwa kabisa na madhila yaliyokuwa yakifanywa na maajinabi dhidi ya Waislamu na ndio maana alikuwa akitumia kiila fursa inayopatikana kwa ajili ya kuwafahamisha watu kuhusiana na hali ya mambo ilivyo.

Moja ya matukio muhimu katika maisha ya Mirza Masih Mujtahid ni fatuwa ambayo aliitoa kwa ajili ya kutetea na kulinda heshima ya Waislamu na kusimama kidete mbele ya dhulma na hujuma za wageni.
Misimamo yake thabiti na kupinga dhulma iliyokuwa ikifanywa na watawala wa wakati huo dhidi ya wananchi Waislamu wa Iran, vilipelekea Mirza Masih Mujtahid abaidishiwe nchini Iraq kwa amri ya watawala. Kusambaa habari ya kutolewa agizo la kubaidishwa Mirza Masih Mujtahid kuliibua hasira na ghadhabu za wananchi. Baada ya hapo kuliibuka maandamanao na mikusanyiko mikubwa ya kupinga kubaidishwa alimu na mwanazuoni huyo. Vyombo vya usalama viliwakandamiza waandamanaji na wananchi waliojitokeza kupinga uamuzi huo. Hatimaye Mirza Mujtahid aliamua kuelekea huko Iraq akiwa na lengo la kuzuia vitendo vya ukandamizaji zaidi dhidi ya raia waliokuwa wakipinga kubaidishwa kwake.
Akiwa kando ya haramu za Najaf na Karbala ambayo yenyewe ilikuwa fursa muhimu, alianza kudhoofika kimwili kutokana na umri mkubwa aliokuwa hasa kutokana na machafuko yaliyokuwa yakiikabili Iraq ambayo yalikuwa yakimpa taabu na mashaka yaliyoambatana na ghamu na huzuni. Hatimaye baada ya kuishi kwa miaka 18 akiwa huko uhamishoni, Mirza Masih Mujtahid Asterabadi aliaga dunia huko Najaf akiwa na umri wa miaka 71. Mwili wa alimu na mwanazuoni huyu mkubwa umezikwa katika haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) mjini Najaf Iraq.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu kwa juma hili, umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mola Karima katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Basi hadi tutakapokutana tena wakati huo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.