Nov 10, 2022 16:59 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (39)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 39 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia Akhlaqi za Kiuchumi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, hakuna shaka yoyote kuwa Uchumi una nafasi muhimu sana katika kuainisha mustakabali na hatima ya jamii na mfumo wowote ule wa utawala; na ndio maana, Uislamu, ambao ni njia ya fikra na dini yenye mtazamo unaozingatia na kujumuisha kila kitu, unaupa uchumi umuhimu mkubwa sana. Kwa maneno mengine ni kwamba, kinyume na wale wenye mitazamo na ufahamu wa kijuujuu wa mambo, Uislamu hauko kama ilivyo sehemu mojawapo ya dini ya Uyahudi inayojali zaidi mali na masuala ya kimaada, wala hauko kama ilivyo sehemu moja ya Ukristo inayojishughulisha na masuala ya kiroho na kiakhlaqi tu. Uislamu, ni dini inayotilia nguvu misingi ya imani na itikadi na wakati huohuo kulipa uzito na umuhimu mkubwa suala la kukidhi mahitaji ya kimaada na kimaisha ya watu. Ili kubainisha umuhimu wa uchumi katika kujenga jamii, aya ya tano ya Suratu-Nisaa inatuasa kwa kusema: "Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Mwenyezi Mungu amekujaalieni kuendeshea maisha…."

Mbali na kuyapa uthabiti maisha ya mtu binafsi, uchumi unaupa nguvu na uwezo wa kujitawala na kujitegemea mfumo wa utawala wa Kiislamu pia. Katika zama mbalimbali na hadi sasa, jamii ya wanadamu imepitia kwenye mifumo tofauti ya uchumi, lakini mfumo wa kiuchumi wa Uislamu una sifa maalumu na za kipekee zinazoupa ubora katika kila hali, kulinganisha na mifumo ya kiuchumi ya Ubepari na Usoshalisti.

Sifa kuu na muhimu zaidi katika hizo, ni misingi miwili ya imani juu ya Mungu, yaani Tauhidi na imani juu ya kufufuliwa, yaani Maadi, ambayo ndiyo inayoipa muelekeo, thamani na malengo mipango yote ya sera na njia za utekelezaji wa uchumi. Kulingana na mtazamo wa kitauhidi kuhusu dunia, ni jambo la kimaumbile na la kawaida kwa mwanadamu kupenda na kuvutiwa na vitu vya ulimwengu uliomzunguka; kwa sababu, hiyo ni hali aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa nayo katika maumbile yake. Katika aya ya 14 ya Suratu-Aal Imran, Qur'ani tukufu inalizungumzia hilo kwa kusema: "Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema." 

Kwa hivyo kwa mtazamo wa Uislamu, kunufaika na nyenzo na suhula za kimaada na za kidunia ni jambo la kawaida na la kimantiki, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyomhutubu Mtume wake katika aya ya 32 ya Suratul A'raf ya kwamba:"Sema: Ni nani aliye haramisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki…."

Nukta muhimu na ya kutiliwa maanani juu ya suala hilo ni kwamba, tujihadhari tusije kwa namna yoyote ile tukatekwa na kuvikumbatia vitu na mapambo hayo ya dunia, kwani kufanya hivyo kutatufanya tushindwe kulifikia lengo la kuumbwa kwetu, ambalo ni kuwa na daraja ya juu kabisa ya ukamilifu wa kiutu.

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba, katika mtazamo wa Uislamu, suhula na vitu vyote vya kimaada na kiuchumi, inapasa vitumiwe kama njia na nyenzo tu; na wala tusivichukulie kuwa ndio ghaya na lengo kuu; kwa sababu katika mtazamo wa Uislamu juu ya dunia, thamani ya kiumbe mwanadamu ni ya juu zaidi kuliko ulimwengu wote wa uumbaji. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Hadithul-Qudsiy ya kwamba: "Nimeumba vitu vyote kwa ajili ya mwanadamu; na nimemuumba yeye kwa ajili yangu Mimi Mwenyewe." Kwa namna fulani, Hadithi hii inabainisha irada na kusudio la Mwenyezi Mungu alipowajibu malaika pale walipomuomba awajuze hekima na falsafa ya kumuumba mwanadamu, kama aya ya 30 ya Suratul Baqarah inavyosema:"Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi)"…

Imam Ali (AS), mwanadamu aliyekamilika na dhihirisho la sifa zote za khalifa wa Mwenyezi Mungu anasema: Muamala mbaya ni wa mtu kuilinganisha nafsi yake na dunia, na kuiweka thamani ya dunia yote kuwa sawa na thamani ya utu wake." Nahjul-Balagha, khutba ya 32

Imam Jaafar Sadiq (AS) ameielezea daraja tukufu na shakhsia iliyotukuka ya Imam Ali (AS) kupitia kinywa chake mwenyewe mtukufu huyo aliposema: "Kwa hakika katika ulimwengu wote, kuna mmoja tu ambaye ninaweza kuifanyia muamala na Yeye, nafsi yangu yenye thamani kubwa na utu wangu wenye hadhi iliyotukuka; na huyo ni Mola wangu. Ghairi ya Yeye, hakuna tena kingine chochote katika ulimwengu, chenye thamani ya kufanyia muamala huo".

Kwa hivyo katika mfumo wa kiuchumi wa Uislamu, msingi wa kumtanguliza Mwenyezi Mungu una nafasi ya kipekee na inapasa mipango na shughuli zote za kiuchumi katika nyanja zote na katika hali yoyote ile iendeshwe kwa msingi wa dini; na hii ndiyo sifa ya kipekee inayodhihirika wazi katika mfumo wa kiuchumi wa Uislamu. Katika aya ya 37 ya Suratu-Nnur, Qur'ani tukufu inaubainisha mtazamo na muelekeo huo kwa kusema: "Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. "

Lakini mbali na hayo, kutokana na mtu mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu kumtambua Yeye Mola kuwa ndiye mmiliki halisi wa ulimwengu, huwa anajihesabu yeye mwenyewe kuwa ni mmliki wa muda, wa kupita na anayetoweka wa kila alichojaaliwa na Mola; na kwa sababu hiyo, kwa upande mmoja, haukumbatii uchumi na mali na kuufanya lengo kuu kwake, wala hazitoi kafara na mhanga thamani za kidini na kiutu kwa sababu ya maslahi na manufaa ya kiuchumi. Na badala ya kutegemea mahesabu tu na uendeshaji wake wa kiuchumi humuelekea Mwenyezi Mungu akiamini kuwa Yeye ndiye Mola, Muumba, Mwendeshaji na Mtoaji riziki kwa viumbe wote; na kila anapokabiliwa na misukosuko ya kiuchumi hutawakali na kumtegemea Yeye, kwa kumwomba ampe auni na msaada katika kila hali na wala haiendekezi nafsi zake ikatekwa na mali na utajiri na kuishia kuwa na jeuri na ghururi. Ni kama isemavyo aya ya sita na ya saba za Suratul-Alaq ya kwamba: "Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri. Akijiona katajirika. " Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 39 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 40 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

 

 

Tags