Nov 17, 2022 10:26 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika sehemu hii ya 3 ya mfululizo wa makala hizi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Wasikilizaji wapenzi, watu wengi wanapigania kubadilisha na kurekebisha jamii zao. Lakini mabadiliko haya hayawezekani kamwe bila ya watu wenyewe kubadilika kwanza. Ubakhili, woga na umaskini ni miongoni mwa vikwazo ambavyo si tu vinamharibu mtu binafsi, bali pia huvuruga uhusiano kati ya mtu binafsi na jamii na kuzuia mageuzi ya mtu binafsi na jamii nzima. Katika moja ya hikma zake, Imam Ali AS anasema:

الْبُخْلُ عَارٌ، وَ الْجُبْنُ مَنْقَصَةٌ، وَ الْفَقْرُ یُخْرِسُ الْفَطِنَ عَنْ [حَاجَتِهِ] حُجَّتِهِ، وَ الْمُقِلُّ غَرِیبٌ فِی بَلْدَتِهِ

Ubakhili ni aibu, na woga ni kasoro, na ufakiri huzuia ulimi wa mwerevu kueleza hoja yake, na maskini ni mgeni katika mji wake.

Ubakhili ni khulka mbaya ambayo inamzuia mtu kutumia kile kilichoko chini ya udhibiti wake na kinyume chake ni ukarimu. Mtu bakhili ni sawa na mtoto mdogo ambaye hayuko tayari kushirikiana na wengine katika vitu vyake vya kuchezea. Hayuko tayari kuwanufaisha wengine kwa zawadi yoyote ya Mungu aliyopewa. Hii ni aibu.

Pia, ubakhili husababisha rasilimali nyingi za kiuchumi za kijamii kwenda nje ya mzunguko sahihi wa kibiashara na kubaki palepale ulipo kwa kiwango kilekile bila ya kuzalisha kitu kipya. Watu mabakhili ni wanyonge sana na hawana uwezo wa kufikiri kijamii kutokana na kung'ang'ania mno mali zao bila ya sababu ya maana, na hii ni aibu nyingine. Imam Ali AS anamshauri Malik Ashtar katika wasia wake maarufu akimwambia. kamwe asimshirikishe mtu bakhili katika washauri wako, kwa sababu bakhili atakushauri uache kutenda haki na atakutia hofu ya ukata na umasikini.

Hofu inapunguza thamani ya uwepo wa mwanadamu. Mtu mwenye woga huwa hajiamini. Huwa hauamini uwezo wake na hujihisi dhaifu mbele ya wengine. Woga humzuia mtu kutumia uwezo wake, ujuzi na vipaji vyake vile ipasavyo. Ndio maana Imam Ali AS hapa anasema, woga ni udhaifu. Haijalishi mtu mwenye hofu ni muumini kiasi gani, lakini huwa hawezi kutenda kama binadamu mkamilifu kwa sababu ya woga wake. Inashangaza, katika barua ya 53 ya Nahj al-Balagha, Imam al Mutaqin Ali bin Abi Talib AS anamshauri Malik Ashtar akimwambia: Kamwe asiwaruhusu watu woga kuingia katika duara la washauri wako.

Amma katika sehemu ya tatu ya hikma tunazozizungumzia leo, Amirul-Muminin Al bin Abi Talib ameashiria tatizo la umasikini na madhara yake ili kuwahimiza Waislamu waendeleze juhudi za kuleta mageuzi katika jamii kwa kusema: Umasikini humfanya mtu mwerevu kuwa bubu na kushindwa kutoa hoja zake hata kama ni za kweli. Umaskini ni moja ya hali ya maisha ambayo watu wengi wamewahi kuionja japo kwa muda mfupi. Wengine wameingizwa kwenye umaskini kidhulma, wengine wamekumbana na hali hiyo kutokana na uvivu au kufikiri vibaya na ziko na sababu nyinginezo. Mtu anapokosa kuwa na muono sahihi na thabiti, umaskini utakuwa na athari mbaya kwake. Popote pale utajiri unapozingatiwa zaidi, basi tambua kuwa hapo pana maskini wanaumia zaidi isipokuwa tu pale matajiri wanapotekeleza ipasavyo majukumu yao. Watu maskini wenye udhaifu wa kufikiri na wenye mawazo finyu, mara nyingi hujiona duni, hata kama kiasili ni watu wenye akili sana. Kutokana na kujiona duni, watu hao huwa wanajizuia kusema na kutetea haki zao. Katika sehemu ya mwisho ya hikma hizi za leo, Imam Ali AS anaongeza kwa kusema: Aliye fukara na mhitaji ni mgeni hata katika mji wake. Kwa sababu mgeni ni mtu asiye na marafiki na ni mtu anayejiona mpweke. Watu wengi duniani huwa hawataki kushirikiana na maskini, hivyo huwaacha kama wageni katika mji wao, tofauti na matajiri, huonekana ni wenyeji katika katika miji ya mbali kutokana na utajiri wao. Kwa ukumbusho huu, Imam Ali AS anawahimiza waumini kujaribu kupambana kikamilifu na umaskini.