Hikma za Nahjul Balagha (4) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 4 ya mfululizo wa makala hizi fupi fupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaendelea kuangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni hikma ya nne.
الْعَجْزُ آفَةٌ، وَ الصَّبْرُ شَجاعَةٌ، وَ الزُّهْدُ ثَرْوَةٌ، وَ الْوَرَعُ جُنَّةٌ، وَ نِعْمَ الْقَرینُ الرِّضی
Kushindwa kufanya kitu ni janga, subira ni ushujaa, zuhdi ni utajiri, uchamungu ni ngao na sahiba bora kabisa ni kuridhika.
Wapenzi wasikilizaji, moja ya siri za mafanikio ya kila mtu katika maisha ni kuwa na roho ya kujiamini na kujithamini. Kujistahi kuna maana ya imani ambayo mtu anakuwa nayo kuhusu thamani na umuhimu wake. Mtu asiyejiheshimu huwa mvivu, maskini na dhaifu na hawezi kutumia uwezo na vipaji vyake vya ndani kulinda heshima yake na kujiletea maendeleo. Mtu dhaifu na anayejidunisha, daima huongozwa na kivuli cha udhaifu na kufeli katika mambo yake. Ndio maana Imam Ali AS akasema mwanzoni mwa hikma yake hii ambayo tunaitupia jicho hapa kwamba: "Ajizi, udhaifu na kutoweza kufanya kitu, ni mdudu na adui mkubwa wa maisha ya mwanadamu." Mtu ambaye ni dhaifu, mwingi wa ajizi na asiye na uwezo wa kufanya lolote ni mwepesi wa kuteleza na ni rahisi kudanganyika na kutoka kwenye njia sahihi. Mtu dhaifu hutiwa hofu na jambo lolote analohisi kuwa lina matatizo. Mtu wa namna hii hupenda sana maisha ya urahisi na ikiwa ataahidiwa pesa na uluwa, hutumia haraka fursa hiyo na yuko tayari kufanya jambo lolote baya. Haja ya kuondokana na janga hili ni kujiheshimu na kujipamba kwa sifa nyingine zinazohitajika za kimaadili, ambazo baadhi yake Imam Ali AS amesema ni ushujaa. Mtu mvumilivu ni mtu wa vitendo na huingia katika utekelezaji wa mambo kishujaa na kivitendo na kusonga mbele. Kwa sababu maisha si njia rahisi na laini bali ni uwanja wa vita. Matatizo muda wote huwashambulia watu kutoka pande zote na ni mwenye subira na mvumilivu tu ndiye anayeweza kushinda vikwazo vyote kwa ushujaa wake.
Sifa nyingine nzuri aliyoizungumzia Imam Ali AS hapa ni kuachana na anasa za duniia. Zuhudi na kuitalikii dunia haimaanishi kutomiliki chochote, bali maana yake ni kuachana na maisha ya anasa na kutotekwa na mapambo ya dunia na kumsahau Muumba. Kwa kweli, zuhudi ni mtaji wa thamani kubwa zaidi kuliko mambo yote ya kidunia. Miongoni mwa sifa kuu za zuhudi ni kujisafisha na hisia za kupenda sana mali na mambo ya kidunia na kuwa imara kiroho kwa kutotegemea mambo ya kilimwengu na kutoshughulishwa na anasa za kidunia. Mtu asiyeshughulishwa na mapambo ya dunia na anayeridhika na alichokadiriwa na Mola wake ndiye tajiri zaidi kuliko watu wote.
Katika hikma hii, Imam Ali AS anasema, uchamungu ni ngao. Alwara'u junnah naam, taqwa na uchamungu ni ngao madhubuti. Ngao ni silaha ya kujihami kwenye medani ya vita dhidi ya mishale au panga na mikuki ya adui. Muumini pia anahitaji ngao katika maisha yake ili kujikinga na majaribu ya kimwili na kiroho.
Imam Ali AS anasema katika sehemu ya tano na ya mwisho ya hikma zake hapa kwamba: ونعْمَ الْقرینُ الرِّضی: kuridhika na kuwa na mtazamo mzuri kuhusu yaliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu ni sahibu na mwenza bora kabisa. Katika hikma hii iliyojaa nuru ya Imam Ali AS, kuridhika na kutosheka na hukumu na qadar ya Mwenyezi Mungu kumefasiriwa na kulinganishwa na sahibu na mwenza mstahiki. Mwanadamu anahitaji sahibu na rafiki katika harakati zake na safari yake ndefu ya kuelekea kwenye ubora na kuwa mwanadamu kamili. Bila ya kuwa na sahibu mwaminifu, huwa ni vigumu kuendelea na safari hiyo bali huwa haiwezekani kabisa. Kutegemea qadar ya Allah hakuna maana ya kujipweteka na kutofanya juhudi zozote, na kusubiri tu kila kitu kifanywe na Mwenyezi Mungu. Hiyo siyo maana kabisa ya kutegemea qadar ya Allah. Sahibu mstahiki ni yule anayempa mtu amani na kumshajiisha kuwa na subira mbele ya matatizo na kumpa roho ya matumaini. Kazi zote hizi ni katika sifa za watu wanaojisalimisha mbele ya qadar na hukumu za Mwenyezi Mungu. Mtu mwenye nafasi hiyo huwa hajigambi, hawi mbishi, huwa imara katika kukabiliana na matatizo, shida na heka heka za maisha ya dunia. Sifa hii nzuri ni moja ya madhihirisho ya imani ya kweli. Mtu ambaye maisha yake yamejaa kuridhika mbele ya hukumu za Allah, kamwe hamuoni kung'unika na kulalamika kwamba mbona wengine wamepata neema hizi na zile yeye hajapata.