Dec 10, 2022 10:40 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 6 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Tali AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

صَدْرُ الْعَاقِلِ‏ صُنْدُوقُ‏ سِرِّهِ‏ وَ الْبَشَاشَةُ حِبَالَةُ الْمَوَدَّةِ وَ الِاحْتِمَالُ قَبْرُ الْعُیُوب

Wasikilizaji wapenzi, Imam Ali AS amesema: Kifua cha mwenye akili ni sanduku la siri zake, na bashasha ni njia ya kuvutia mapenzi na marafiki, na uvumilivu hufunika makosa na mapungufu ya mtu.

Kujumuika na kuingiliana na watu, kutafuta marafiki wazuri na kudumu nao katika ulimwengu huu wa leo uliopiga hatua kubwa za kimaendeleo na hata katika nyakati za zamani zilizokuwa hazina teknolojia yoyote, suala la kupata marafiki wazuri na kudumu nao lilikuwa ni daghadagha ya wanadamu wote. Imam Ali AS, katika hikma hii ya sita ya Nahjul Balagha anaeleza nukta chache za kutatua matatizo hayo. Kifua cha mwenye akili na hikma, ni kifua kipana sana. Ni kifua cha muungwana. Ni kifua chenye busara. Ni kama sanduku la kuhifadhia siri zake mtu. Kuwa na bashasha pia ni njia ya kuwafanya watu wakupende. Ni njia ya kupata marafiki, na subira na uvumilivu hufunika makosa na mapungufu ya mtu.

 

Naam, moyo wa mtu ni sanduku la hazina la siri zake. Ufunguo wa kufungulia sanduku hilo ni ulimi. Huo ni mfananisho wa mahala pake kabisa, kwani mara nyingi tunapotaka kumhakikishia mtu kwamba hatutatoa siri yake, tunasema; Ninaiweka moyoni mwangu sitoruhusu ulimi wangu kumhadithia yeyote. Ni kwa sababu hii ndio maana hapa Imam Ali AS anauita moyo kuwa sanduku la kuhifadhia siri. Moyo ni mahali salama ambapo vitu vya thamani hutunzwa ndani yake, ili mtu yeyote asiweze kuvipata. Siri za watu ni moja ya vitu vya thamani kubwa sana ambavyo havipaswi kupewa kila mtu. 

Watu wengine wana tabia za kuwafichulia watu wengine siri zao mara tu wanapokuwa marafiki. Wakati ukweli ni kwamba, urafiki mwingi huwa ni wa muda mfupi na inatokezea sana tu marafiki wakubwa wa leo, kesho wakawa maadui wa kupigana risasi. Mtu anapofichua siri yake huwa anajianika kwa watu wengine na kuwafanya wajue udhaifu wake wa ndani. Suala hili lenyewe hudhoofisha na kuteteresha msingi wa urafiki. Kwa hiyo, ikiwa mtu mwenye hekima anataka urafiki wake ubaki kwenye kilele cha heshima, hana njia nyingine isipokuwa kuweka siri yake moyoni mwake na kutowaeleza wengine siri yake na asiwe na tabia ya kufichua siri za wengine. Kwa kujipamba na tabia hiyo ndipo ataweza kuvutia wengine wapende kufanya urafiki naye. 

 

Pembeni mwa kutunza siri, kuna hili suala la bashasha na uchangamfu mbele ya wengine. Hili pia ni njia nzuri ya kuvutia kupendwa na wengine na kupata mafariki wazuri. Kama tunavyojua, kupata rafiki mzuri na mwema si kazi rahisi. Baadhi ya marafiki wamefananishwa na ndege ambao ni lazima ufanye bidii kubwa kuweza kuwapata. Imam Ali AS amesema, njia bora na isiyo na gharama kubwa ni mtu kuwa mwema. Kutenda wema ni kama mshipi wa kuvulia samaki. Kutabasamu hufanya uso wa mtu kuwa mzuri na wa kuvutia. Kwa hiyo, njia bora ni mtu kujipamba kwa tabia nzuri tangu akiwa bado mtoto mdogo ili athari yake ya ajabu iweze kuonekana katika maisha yake yote na ya wanajamii wenzake.

Jambo lingine muhimu la kuimarisha urafiki na usuhuba, ni kuvumiliana makosa na mapungufu ya kila upande. Jambo hilo si muhimu tu katika kuimarisha marafiki, lakini pia ni muhimu sana katika kuwavutia wengine kujiunga na urafiki wa wawili hao. Kwa sababu hii, unapaswa kuvumilia makosa na mapunguvu ya rafiki yako kwa busara na hekima kubwa. Hakuna mtu asiye na kasoro. Ni bora kuvumilia mapungufu ya wenzako kwa kuzingatia uhakika huo kwamba mwanadamu si mkamilifu. Ayatullah Seyyed Abul Qasim Khoei, mmoja wa wanazuoni wakkubwa wa karne hii ametoa ufafanuzi kuhusu hikma hii ya Imam Ali AS akisema: “Kama ambavyo mtu anapofariki dunia hufukiwa kaburi ili kuficha uvundo wa maiti yake na kuhifadhi heshima yake, kuvumilia mapungufu ya mwezako huficha kasoro za matendo na tabia mbaya za mtu mbele ya wengine. Tab'an, kuvumilia makosa ya marafiki hakuondoi jukumu la kujaribu kumrekebisha anapokosea. Ndio maana Imam Ali AS amenukuliwa akisema: Mtu anayedai kuwa ni rafiki yako lakini haonyeshi makosa yako pamoja na kwamba anayaona, huyo si rafiki wa kweli.