Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Disemba 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Mfunguo Nane Jumad al-Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 22 Disemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 2168 iliyopita, duru ya tatu na ya mwisho ya vita vya kihistoria na vya umwagaji damu kati ya tawala za kifalme za Carthage na Roma ilimalizika kwa kupata ushindi Waroma na kuanguka utawala wa Wacartharge. Vita vya falme hizo mbili vilijulikana kwa jina mashuhuri la vita vya Punic. Utawala wa kifalme wa Carthage ulikuwa moja kati ya tamaduni kongwe huko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Mediterrania.
Miaka 383 iliyopita katika tarehe kama ya leo, alizaliwa Jean Racine malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kifaransa. Racine alianza kazi ya uandishi katika uwanja huo baada ya kusoma kwa muda fulani na kuhitimu akiwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo muda fulani baadaye alianza kukosoa kazi hiyo baada ya kuandika mchezo wa tanzia alioupa jina la Andromaque na kupata umashuhuri. Alianza kuakisi matukio ya mfalme wa wakati huo wa Ufaransa. Jean Racine alifariki dunia mwaka 1699 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 329 iliyopita, ulitokea mtetemeko mkubwa wa ardhi katika kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Kufuatia zilzala hiyo, miji mitatu mikubwa ya kisiwa hicho ilibomolewa na kusababisha hasara kubwa kwa miji mingine yakiwemo makao makuu ya kisiwa hicho yaani Palermo. Mtetemeko huo wa ardhi unahesabiwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Italia. Zaidi ya watu 80,000 walipoteza maisha yao katika janga hilo la kimaumbile.

Siku kama ya leo miaka 266 iliyopita, aliaga dunia Abdul Karim bin Ahmad Halabi mpokezi wa hadithi wa Kiislamu. Alikuwa mashuhuri mno katika upokezi wa hadithi katika zama zake katika mji wa Halab unaopatikana hii leo huko nchini Syria. Halabi alisoma elimu za Fiqh, Usuul al-Fiqh, tafsiri, hadithi na elimu nyingine zilizokuwako katika zama zake kwa baba yake na maulama wengine. Baadaye Halabi alikuwa kipofu ingawa hata hivyo hakupoteza moyo wa matumaini aliokuwa nao na aliendelea kujihusisha na elimu ya hadithi. Msomi huyo ana vitabu mbalimbali na kimojawapo ni kile kinachoitwa Ad'ayat Safar.

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Ufaransa na Uingereza zilihitimisha udhibiti wao wa siku 50 wa bandari ya Port Said nchini Misri na kutoa majeshi yao katika bandari hiyo. Inafaa kuashiria hapa kwamba, baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulio katika jangwa la Sinai, mashambulio ya pamoja ya anga ya Uingereza na Ufaransa dhidi ya Misri nayo yalianza. Mashambulio hayo, yalisababisha hasara kubwa katika Mfereji wa Suez. Sababu ya kufanywa mashambulio hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kama Vita vya Mfereji wa Suez, ni hatua ya Rais Gamal Abdul-Nassir wa Misri ya kutangaza kutaifisha mfereji huo. Umoja wa Mataifa uliiunga mkono Misri wakati wa mashambulio hayo, na kwa utaratibu huo tawala tatu hizo, yaani Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel zikaondoa majeshi yao katika ardhi ya nchi hiyo.
Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita yaani tarehe 22 Disemba mwaka 1989 Miladia, uongozi wa Nicolae Ceausescu, Rais na Mkuu wa chama cha Kikomonisti cha Romania uliangushwa na siku tatu baadaye kiongozi huyo pamoja na mkewe wakanyongwa. Mke wa Ceausescu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri wa serikali ya Romania. Rais huyo wa zamani wa Romania ya kidikteta aliasisi chama hicho cha Kikomonisti kama walivyofanya watawala wengine wa nchi za Kisoshalisti za Ulaya.