Dec 24, 2022 06:17 UTC
  • Jumamosi, 24 Disemba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1444 Hijria mwafaka na tarehe 24 Disemba 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1139 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Muhammad bin Othman bin Said Amri Naibu wa pili maalumu wa Imam Mahdi (atfs). Alichukuua jukumu hilo, baada ya kuaga dunia baba yake yaani Othman bin Said aliyekuwa naibu wa kwanza maalumu wa Imam Mahdi (atfs). Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad bin Said alikuwa akiaminiwa na Ahlul-Bayt (as0 na katika kipindi cha miaka 40 cha kushikilia wadhifa wake, licha ya kukabiliwa na mbinyo wa Bani Abbas lakini, aliweza kutekeleza vyema jukumu lake. ***

Miaka 498 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498 baharia huyo wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India. ***

Miaka 173 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya Ufaransa yaliishambulia ardhi ya Guinea ya magharibi mwa Afrika. Mashambulio hayo yalikuwa utangulizi wa Ufaransa kudhibiti ardhi hiyo iliyokuwa na utajiri wa dhahabu. Kabla ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia ardhi ya Guinea, kulikuwa kumeanzishwa mashirika ya kibiasharaya dhahabu katika pwani ya Guinea. ***

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi. Hata kama kundi la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limeshafanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao. ***

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi kuteuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Miladia Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951. ***

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Ayatullah Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein. ***