Jun 14, 2016 23:54 UTC
  • Jumatano, Juni 15, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 9 Ramadhani mwaka 1437 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Juni mwaka 2016.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani alimu na marja mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum huko kusini mwa Tehran. Ayatullah Lankarani alianza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana ambapo alistafidi na mafunzo ya walimu wakubwa kama vile Ayatullahil udhma Burujerdi na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani katika kipindi kifupi aliweza kufikia daraja ya ijtihad.

Tarehe 15 Juni miaka 168 iliyopita Kansela wa Ujerumani wa wakati huo aliufanya mji wa kihistoria na mashuhuri wa Berlin kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuchaguliwa Berlin kuwa kituo cha utawala wa Ujerumani kulifanyika baada ya kutekelezwa mpango wa kuiunganisha Ujerumani, ambao mwasisi wake alikuwa Bismark.

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamedani. Alikuwa miongoni mwa maulamaa na wanazuoni wakubwa wa karne ya 13 na 14 Hijria Qamaria nchini Iran na alisifika kwa kuwa na takwa na uchamungu.Baada ya kukamilisha masomo ya msingi na kati, Ayatullah Hamedani alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu na alianza kufunza na kueneza elimu baada ya kukamilisha masomo yake. Vitabu vyake vimekusanywa katika majmui iliyopewa jina la 'Tadhkiratul Muttaqiin'.

Na tarehe 15 Juni miaka 308 iliyopita harakati ya wapigania uhuru wa Scotland ilikandamizwa vikali na Uingereza. Uingereza daima imekuwa ikifanya jitihada za kuiunganisha Scotland na ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo harakati za mapambano za Wascotland zilipinga vikali suala hilo. Hata hivyo mwaka 1707 mabunge ya nchi hizo mbili yaliunganishwa. Suala hilo liliwakasirisha sana Wascotland walioanzisha harakati nyingine ya mapambano mbayo ilikandamizwa vikali katika siku kama ya leo hapo mwaka 1708.