Jan 07, 2023 02:36 UTC
  • Jumamosi, 07 Januari, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Tisa Jamaduthani 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 7 Januari 2023 Miladia.

Siku inayosadifiana na hii ya leo, miaka 132 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti mmoja kati ya wanazuoni na maraaji' wakubwa wa Kiislamu. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti taratibu akawa mmoja wa maraaji' wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Badaiul Afkar. ***

Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti

 

Miaka 87 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wanawake wa Kiirani walipigwa marufuku kuvaa vazi la Kiislamu la aina yoyote kufuatia amri ya Ridhakhan Pahlavi. Ridhakhan alitoa amri hiyo baada ya kutekelezwa mpango wa kubadili mavazi ya wanaume nchini Iran. Mpango huo ulitekelezwa kwa lengo la kufuta thamani za Kiislamu na badala yake kuiga utamaduni wa Kimagharibi. Ridhakhan alitekeleza mpango huo wa kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu nchini Iran baada ya safari yake nchini Uturuki na kufuata nyayo za Kemal Atatürk Rais wa wakati huo wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi ambaye aliwapiga marufuku wanawake wa nchi hiyo kuvaa mavazi ya Kiislamu. ***

Reza Khan

 

Miaka 80 iliyopita yaani mnamo tarehe 7 mwezi Januari mwaka 1943 aliaga dunia Nikola Tesla mwanafikia mzaliwa waYugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux). ***

Nikola Tesla

 

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita,  Gholamreza Takhti mchezaji na bingwa wa mchezo wa mieleka wa Kiirani aliuawa kwa njama zilizopangwa na utawala wa wakati huo wa Shah. Takhti Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa na maisha ya kati na kati. Gholamreza Takhti alijulikana mno kwa tabia yake ya huruma, ukweli na mapenzi yake kwa watu.  Katika kipindi cha uhai wake na wakati wa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, Gholamreza Takhti alifanikiwa kuipatia Iran medali 9 za dhahabu na fedha katika mashindano ya Olimpiki. Takhti ni miongoni mwa wachezaji wa Kiirani waliotwaa medali nyingi za dhahabu na fedha katika mashindano muhimu ya kimataifa. ***

Gholamreza Takhti

 

Tarehe 17 Dei miaka 45 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran. ***

Imam Khomeini

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita,  majeshi ya Vietnam yaliishambulia Cambodia na kupelekea dikteta wa nchi hiyo Pol Pot kuikimbia nchi hiyo na hatamu za uongozi kuchukuliwa na Heng Samrin. Pol Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge la Cambodia lililokuwa likifuata fikra za Kimao. Katika kipindi cha chini ya miaka mitatu cha uongozi wake nchini Cambodia, Pol Pot akishirikiana na kundi la Khmer Rouge aliwauwa watu kati ya milioni 1.5 na milioni 2.  ***

Pol Pot

 

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Suleiman Khater mmoja wa polisi wa mpakani katika jangwa la Sinai, alikufa shahidi akiwa jela. Akionyesha upinzani wake dhidi ya mkataba wa Camp David, Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni kadhaa katika jangwa la Sinai. Serikali ya Misri baada ya kumtia mbaroni askari huyo, ilimhukumu kifungo cha maisha jela. Hata hivyo baada ya muda kiwiliwili cha Suleiman Khater kilipatikana katika kituo cha matibabu cha magereza kikiwa kimening'inia na serikali ya Misri ilidai kwamba, mfungwa huyo alijiuwa. ***

Suleiman Khater