Jun 16, 2016 04:26 UTC
  •  Alkhamisi 16 Juni 2016.

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Ramadhani 1437 Hijria sawa na tarehe 16 Juni 2016.

 

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, iliyopita alifariki dunia Bi Khadija binti Khuwailid, mke wa Mtume Muhammad SAW katika mji wa Makka. Bi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka aliolewa na Mtume Mtukufu miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad SAW na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Kiislamu. Kuweko Bi Khadija SA pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume SAW alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa. Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib ami yake Mtume SAW pia alifariki dunia mwaka huo huo.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Khordad 1358 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuanzishwa Jihad ya Ujenzi wa taifa kwa lengo la kujitawala na kujitosheleza taifa la Iran na kujikwamua na umasikini na matatizo mbalimbali hasa vijijini. Kufuatia amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wanachuo na vijana wenye imani na wasomi waliungana ili kujenga na kukarabati maeneo yaliyokuwa duni na yaliyokuwa nyuma kimaendeleo. Jihadi ya ujenzi wa taifa ambayo ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu ilibadilisha sura ya maeneo mbalimbali duni nchini, kutokana na hatua muhimu zilizochukuliwa za ujenzi wa miundo mbinu. Baadaye jihadi ya ujenzi ilibadilishwa na kuwa wizara na kisha kuunganishwa na wizara ya kilimo na kuwa Wizara ya Jihadi ya Kilimo.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.

Na siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.